Rais wa DRC: Hospitali Kinshasa zimefurika wagonjwa wa Corona
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i71226-rais_wa_drc_hospitali_kinshasa_zimefurika_wagonjwa_wa_corona
Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametahadharisha kuwa, nchi hiyo huenda ikakabiliwa na maafa makubwa katika wimbi la tatu la maambukizi ya virusi vya Corona.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 14, 2021 02:23 UTC
  • Felix Tshisekedi
    Felix Tshisekedi

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametahadharisha kuwa, nchi hiyo huenda ikakabiliwa na maafa makubwa katika wimbi la tatu la maambukizi ya virusi vya Corona.

Tshisekedi amesema nchi hiyo imesajili idadi ya kutisha ya vifo na kesi mpya za maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 katika siku za hivi karibuni, na amewataka wananchi kuwa makini na kuzingatia maagizo ya Wizara ya Afya ya kudhibiti msambao wa virusi hivyo.

Rais Tshisekedi amesema hospitali na vituo vya afya nchini humo hususan katika mji mkuu, Kinshasa vimefurika wagonjwa wapya wa Corona.

Ameonya kuwa, "wimbi hili linaonekana kuwa hatari kuliko wimbi la kwanza na la pili, na kwa msingi huo sheria kali za kudhibiti msambao wa virusi hivyo zinapaswa kuwekwa."

Kadhalika ametangaza kufutwa sherehe za kumbukumbu na kumuezi Patrice Lumumba, Waziri Mkuu wa kwanza kuchaguliwa kwa njia ya demokrasia nchini humo, zilizopaswa kufanyika mwezi huu wa Juni. Amesema maadhimisho hayo sasa yatafanyika Januari mwaka ujao 2022.

Mkongomani akipimwa joto la mwili

Haya yanajiri huku nchi kadhaa za Afrika kama Uganda na Zambia zikiripoti pia ongezeko kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19. Wiki iliyopita, Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliagiza shule zote zifungwe nchini humo kama hatua ya kuzuia maambukizi zaidi ya Covid-19.

Hadi sasa nchi za bara la Afrika ambazo zinakabiliwa na uhaba na ukosefu wa chanjo za Covid-19, zimerekodi kesi zaidi ya milioni tano za Corona, na vifo zaidi ya 134,000 vya maradhi hayo. Aidha wagojwa zaidi ya milioni 4 na laki 5 wa Corona barani humo wamepata afueni.