Jul 25, 2021 01:19 UTC
  • Wanajeshi saba wa Cameroon wauawa katika shambulio la Boko Haram

Wanajeshi wasiopungua saba wa Cameroon wameuawa baada ya wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram kushambulia kambi moja ya kijeshi kaskazini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Duru za kiusalama nchini Cameroon zimethibitisha kutokea shambulio hilo la mauaji lililotekelezwa na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram alfajiri ya jana Jumamosi eneo la Sagme katika jimbo la Far North.

Askari mmoja ameliambia shirika la habari la Xinhua kuwa, wanachama hao wa Boko Haram waliwasili kambini hapo wakiwa wamevalia magwanda ya kijeshi na kuanza kufyatua risasi ovyo. Makabiliano ya risasi yalijiri kwa masaa kadhaa.

Habari zaidi zinasema kuwa, kamanda aliyekuwa akiisimamia kambi hiyo ya jeshi la Cameroon ni miongoni mwa askari waliouawa katika hujuma hiyo inayosemekana kuwa mbaya zaidi dhidi ya maafisa usalama nchini humo katika kipindi cha miezi kumi.

Mapema mwaka huu 2021, watu wasiopungua 13 waliuawa nchini Cameroon na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya kundi la kigaidi la Boko Haram kufanya shambulio kaskazini mwa nchi hiyo.

Askari wa Cameroon

Duru za kiusalama zinaarifu kuwa, watu zaidi ya 2,000 wameuawa tangu genge hilo la ukufurishaji lianzishe harakati na mashambulio yake katika eneo la Far North la kaskazini mwa Cameroon mwaka 2014. 

Kundi la kigaidi la Boko Haram lilishika silaha mwaka 2009 kwa lengo la kile lilichotaja kuwa, kuwa huru eneo la kaskazini mwa Nigeria; na kuanzia hapo likaanza kueneza jinai na mashambulizi yake huko Niger, Chad na kaskazini mwa Cameroon.

 

Tags