Sep 12, 2021 03:07 UTC
  • Matukio ya kisiasa ya Morocco; Mohammed VI ateua waziri mkuu mpya

Baada ya kushindwa vibaya chama tawala cha Uadilifu na Ustawi (PJD) katika uchaguzi wa wiki iliyopta nchini Morocco, Mfalme Mohammed VI wa nchi hiyo amemteua Aziz Akhannouch wa chama cha National Rally of Independents (NRI) kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo. Akhannouch amepewa jukumu la kuunda serikali mpya ya Rabat.

Kabla ya uchaguzi wa karibuni wa Morocco, ilitazamiwa kuwa chama cha PJD kingeibuka na ushindi. Chama hicho kimekuwa na nafasi kubwa katika uwanja wa siasa wa Morocco baada ya kushinda awamu mbili za uchaguzi wa Bunge wa mwaka 2011 na 2016. Hata hivyo kinyume na makadirio ya wachambuzi wa mambo, chama tawala cha The Justice and Development Party (PJD) kilichokuwa na viti 125 kimepata pigo kubwa na kuambulia 12 tu, kikiwa nyuma sana ya wapinzani wake wakuu, National Rally of Independents (NRI), Authenticity and Modernity Party (PAM), na chama cha Istiqlal (PI). 

Baada ya kupigwa mweleka na kuangukia pua, chama cha PJD kimedai kuwa, uchaguzi huo umechakachuliwa na kwamba kumefanyika uhalifu na ukiukaji wa sheria katika majimbo mengi ya uchaguzi. Vilevile viongozi wa chama hicho akiwemo Katibu Mkuu, Saad Eddine El Othmani, wametangaza kujiuzulu baada ya kushindwa vibaya katika uchaguzi wa Bunge kwa kuambulia viti 12 tu. Taarifa iliyotolewa na chama hicho imesema, matokeo yaliyotangazwa hayaeleweki, si ya kimantiki na wala hayaakisi ramani halisi ya kisiasa na nafasi ya chama cha PJD katika medani ya siasa ya Morocco.

 Saad Eddine El Othmani

Weledi wa mambo wanasema, hali isiyofaa ya kisiasa na kiuchumi ya jamii ya Morocco ni miongoni mwa sababu la kulambishwa odongo chama tawala cha PJD. Sababu nyingine ya kushindwa chama hicho ni hatua ya serikali ya Rabat ya kusaini mapatano ya amani na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuwasaliti watu wanaodhulumiwa wa Palestina. Baada ya Imarati, Bahrain na Sudan, Morocco ilikuwa nchi ya nne ya Kiarabu kutia saini makubaliano ya kuanzia uhusiano wa kidiplomaia na utawala wa Kizayuni chini ya mashinikizo ya aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump. Uchunguzi wa maoni ulionesha kuwa, baada tu ya Morocco kusaini mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel asilimia 88 ya Wamorocco walipinga hatua hiyo.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Kupambana na Mwenendo wa Kuanzisha Uhusiano na Israel nchini Morocco anasema kuwa: "Chama tawala cha PJD kimelipa gharama ya kuwasaliti Wapalestina kwa kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Tel Aviv."

Serikali mpya ya Morocco imechukua hatamu za uongozi huku nchi hiyo ikisumbuliwa na migogoro mingi ya ndani na katika siasa za nje.

Hatu ya Rabat ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel na safari za mara kwa mara za viongozi wa serikali ya Tel Aviv nchini Morocco vimewakasirisha sana wananchi wa nchi hiyo. Katika upande mwingine machafuko ya maeneo ya mpakani, kukatwa uhusiano wa Morocco na Algeria na mgogoro wa kisiasa unaoendelea kutokota baina ya nchi hizo mbili vimezisha hali ya wasiwasi na mtikisiko katika siasa za nje za Rabat. Vilevile moto mkubwa uliotokea nchini Algeria ambao Algiers inasema uliwashwa kwa makusudi na makundi yanayoungwa mkono na kusaidiwa na Morocco na Israel, vimezidisha hali ya mvutano katika uhusiano wa pande hizo mbili.

Pamoja na hayo yote inaonekana kuwa, kuteuliwa Aziz Akhannouch kuwa Waziri Mkuu mpya wa Morocco hakutakuwa na mabadiliko yoyote katika hali ya sasa ya nchi hiyo.

Akhannouch anahesabiwa kuwa miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa suala la kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel na ana uhusiano mkubwa na washirika wa Ulaya wa serikali ya Rabat. Vilevile anahesabiwa kuwa miongoni mwa vibopa na matajiri wakubwa wa Morocco wenye uhusiano wa karibu sana na Mfalme Mohammed VI.

Hata hivyo kushindwa vibaya chama cha Uadilifu na Ustawi (PJD) katika uchaguzi wa karibuni wa Bunge kumeonesha kuwa, kuendelezwa siasa za sasa kutakifanya chama cha National Rally of Independents (NRI) na serikali yake ikabiliwe na hatima ileile ya chama cha PJD.       

Tags