Sep 23, 2021 08:06 UTC
  • Algeria yaizuia Morocco kupita katika anga yake; uhusiano wazidi kuharibika

Serikali ya Algeria imetangaza kuwa, imeifungia Morocco anga yake hatua ambayo inazidi kuchochea mvutano ulioshadidi hivi karibuni baina ya majirani hao wawili kufuatia hatua ya Algiers ya kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Rabat.

Uamuzi huo umetangaza na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Algeria ambalo limetoa agizo la kuifungia Morocco mara moja anga ya Algeria. Hii ina maana kwamba, ndege za abiria na zisizo za abiria za Morocco haziruhusiwa kupita katika anga ya Algeria.

Baada ya kushadidi mvutano baina ya nchi hizo mbili jirani za Kiarabu za Afrika Kaskazini huku ikiaminika kuwa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umekuwa na nafasi katika kadhia hiyo, mwezi uliopita wa Agosti Algeria ilichukua hatua ya kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Morocco ikiituhumu Rabat kuwa imehusika na hatua kadhaa za kiuadui na kiuhasama dhidi yake.

Kiwango cha sasa cha mivutano na mikwaruzano baina ya Algeria na Morocco hakijawahi kushuhudiwa kwa zaidi ya miaka 20.

Ramtane Lamamra, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Algeria

 

Tukio la moto mkubwa uliosambaa kwenye misitu ya Algeria ambalo lilisababisha vifo vya watu wasiopungua 90 na kuwajeruhi wengine wengi na sisitizo la viongozi wa Algiers kwamba ajali hiyo ilisababishwa makusudi kwa kuhusisha makundi ya kigaidi, linatajwa kuwa, limeshadidisha hali ya mvutano iliyokuwepo baina ya nchi hiyo na Morocco.

Aidha hatua ya serikali ya Morocco ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel inaelezwa kuwa, sababu nyingine ya kuharibika uhusiano baina ya nchi mbili hizo kwani Algeria imechukizwa mno na kitendo cha jirani yake huyo.

Tags