Mashambulio ya waasi yalazimisha watu 100,000 kukimbia makazi yao DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i75800-mashambulio_ya_waasi_yalazimisha_watu_100_000_kukimbia_makazi_yao_drc
Mashambulio ya mara kwa mara ya magenge ya waasi yamewalazimisha watu zaidi ya 100,000 kukimbia makazi yao katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 15, 2021 23:02 UTC
  • Mashambulio ya waasi yalazimisha watu 100,000 kukimbia makazi yao DRC

Mashambulio ya mara kwa mara ya magenge ya waasi yamewalazimisha watu zaidi ya 100,000 kukimbia makazi yao katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hayo yalisemwa jana Ijumaa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ambayo imefafanua kuwa, kuanzia Septemba 23 hadi sasa, asilimia 95 ya wakazi wa vijiji vya Komanda na Makayanga katika eneo la Irumu mkoani Ituri mashariki mwa Kongo DR wameyakimbia makazi yao kutokana na hujuma hizo za waasi.

OCHA imeeleza kuwa, watu hao waliokimbia makazi yao hivi sasa wameenea katika vijiji vya Marabo, Nyakunde, Mungamba, Lolwa, na Biakato. 

Taarifa ya OCHA imeongeza kuwa, wakimbizi hao wa ndani wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha, huku wakisumbuliwa na ukosefu wa chakula, maji, makazi na hata dawa.

Wakimbizi wa ndani mkoani Ituri DRC wanavyosakamwa na hali ngumu ya maisha

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya watu wasiopungua 13 kuuawa katika eneo la Oicha mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kufuatia mashambulio ya waasi wa Uganda wa ADF.

Kundi hilo la waasi linalotokea kaskazini mashariki mwa Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu muongo wa 90, ambapo limeua mamia ya watu, mbali na kupelekea malaki ya wengine kuwa wakimbizi.