Jeshi la Kongo: Tumekomboa maeneo yote kutoka mikononi mwa M23
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza kuwa limekomboa maeneo yote ambayo Jumapili wiki iliyopita yalishambuliwa na waasi wa zamani wa kundi la Machi 23 mashariki mwa nchi hiyo.
Jeshi la Kongo awali liliwatuhumu waasi hao wa zamani wa kundi la M23 kuwa wameishambulia kambi yake katika eneo la Rutshuru mashariki mwa nchi hiyo na kwamba mapigano yalikuwa yakiendelea dhidi ya waasi hao wa zamani wa M23. Jenerali Sylvain Ekenge Naibu Msemaji wa Jeshi la Kongo (FARDC) amesema kuwa waasi hao wa zamani wa M23 walizishambulia ngome zao huko Rushuru kwa lengo la kuyumbisha hali ya usalama katika eneo hilo.
Amesema M23 walishambulia maeneo ya mbali katika vijiji vya Runyonyi na Chanzu katika miinuko ya kistratejia kati ya Rwanda na Uganda katika mkoa wa Kivu Kusini. Kupitia taarifa yao ya Jumatatu wiki hii waasi hao wa zamani wa M23 walikanusha kuwa kundi lao halihusiki na mashambuli hayo tajwa au kupigana vita na jeshi au serikali.
Shirika la Msalaba Mwekundu la Uganda limeripoti kuwa, mapigano yaliyojiri kati ya makundi yenye silaha yamesababisha wimbi la watu kukimbilia Uganda. Limeongeza kuwa, tayari limetuma timu ya wataalamu kutathmini mahitaji mbalimbali ya raia waliokimbia mapigano kati ya makundi yenye silaha yasiyofahamika. Irene Nakasiita Msemaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Uganda amesema kuwa mamia ya watu sasa wamepiga kambi kwa muda katika kivuko cha mpakani cha Bunagana wakitafuta makazi Uganda.