Makumi wauawa katika mashambulizi ya waasi wa CODECO, DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i77222-makumi_wauawa_katika_mashambulizi_ya_waasi_wa_codeco_drc
Makumi ya watu wameuawa katika mashambulizi mapya ya kutisha ya wanamgambo wa CODECO huko kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 23, 2021 04:07 UTC
  • Makumi wauawa katika mashambulizi ya waasi wa CODECO, DRC

Makumi ya watu wameuawa katika mashambulizi mapya ya kutisha ya wanamgambo wa CODECO huko kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Shirika la Kivu Security Tracker linalofuatilia ghasia na mapigano mashariki mwa DRC limesema, maiti 107 zimepatikana katika vijiji viwili vya  Drodro na Largu katika eneo la Djugu mkoani Ituri kufuatia hujuma hizo za juzi Jumapili na jana Jumatatu.

Taarifa ya taasisi hiyo ya kiraia imefafanua kuwa, aghalabu ya maiti hizo ni za raia na kwamba, waasi hao wa CODECO walilenga makazi ya wakimbizi wa ndani katika maeneo hayo.

Wakazi wa vijiji hivyo wanasema umwagaji damu huo umefanyika kwa kiwango hicho cha kuogofya kwa kuwa jeshi la DRC lilichelewa kufika katika maeneo ya tukio lilipoitwa na wananchi.

Utitiri wa magenge ya waasi DRC

Hata hivyo, kwa mujibu wa Jules Ngongo, Msemaji wa Jeshi la DRC katika mkoa wa Ituri ni kwamba, watu waliouawa katika hujuma hizo ni 12. Amesema waliouawa katika mashambulio hayo ni watoto sita, wanaume wanne na wanawake wawili.

Wiki iliyopita,  Shirika la Kivu Security Tracker lilitangaza kuwa, kwa akali raia 1,137 wameuawa katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri, tangu Rais Felix Tshisekedi wa nchi hiyo alipotangaza 'hali ya mzingiro' katika maeneo hayo mawili mwezi Mei.