Zimbabwe yaathiriwa na wimbi la kuhajiri wafanyakazi wa sekta ya afya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i78120-zimbabwe_yaathiriwa_na_wimbi_la_kuhajiri_wafanyakazi_wa_sekta_ya_afya
Zimbabwe imeathiriwa na wimbi kubwa la wafanyakazi wake wa sekta ya afya kuhajiri na kwenda nchi za nje kutafuta kazi wakati huu ambapo nchi hiyo inasumbuliwa pakubwa na maambukizi ya VOVID-19. Hadi sasa zaidi ya wafanyakazi wa sekta ya afya 2,200 wameondoka Zimbabwe na kuelekea Marekani, Uingereza, Australia na katika mataifa jirani kwa ajili ya kusaka ajira.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 17, 2021 03:04 UTC
  • Zimbabwe yaathiriwa na wimbi la kuhajiri wafanyakazi wa sekta ya afya

Zimbabwe imeathiriwa na wimbi kubwa la wafanyakazi wake wa sekta ya afya kuhajiri na kwenda nchi za nje kutafuta kazi wakati huu ambapo nchi hiyo inasumbuliwa pakubwa na maambukizi ya VOVID-19. Hadi sasa zaidi ya wafanyakazi wa sekta ya afya 2,200 wameondoka Zimbabwe na kuelekea Marekani, Uingereza, Australia na katika mataifa jirani kwa ajili ya kusaka ajira.

Bodi ya Huduma za Afya ya Serikali ya Zimbabwe imeeleza kuwa, idadi hiyo ni zaidi ya mara mbili ya idadi ya madaktari, wauguzi na wafamasia ambao mwaka jana waliondoka nchini humo, na mara tatu ya wale walioondoka Zimbabwe mwaka 2019. 

Maafisa Zimbabwe wameeleza kuwa wimbi hilo la kuhajiri na kwenda nje kutafuta kazi limeathiri mfumo dhaifu wa afya wa Zimbabwe ambao unakabiliwa na uhaba wa suhula za tiba na madawa. 

Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza kuwa madaktari wapatao 23 watoe huduma kwa watu elfu kumi; jambo ambalo Zimbabwe bado iko mbali sana kulitimiza. Utafiti wa mwisho uliofanywa mwaka 2015 ulionyesha kuwepo wastani wa madaktari 1.6 tu kwa kila watu 10,000 nchini Zimbabwe.

Wahudumu wa afya Zimbabwe wanahama nchi kufatuta maisha bora

Mishahara ya madaktari na wataalamu wa afya nchini Zimbabwe imeendelea kuwa chini licha ya serikali ya Harare kuahidi kuboresha mishahara yao. Mfanyikazi wa kawaida katika sekta ya umma nchini humo hupokea mshahara wa chini ya dola 200 za Kimarekani kwa mwezi, wakati nchini Uingereza - ambayo ililegeza vizuizi vya visa kwa wafanyikazi wa afya mnamo 2020 - wanaweza kupata mara 10 zaidi.