Zaidi ya magaidi 80 wauawa Sinai, Misri
Jeshi la Misri limetangaza kuwa, limefanikiwa kuua magaidi wasiopungua 85 katika kipindi cha siku nne zilizopita kwenye maeneo ya Sheikh Zuweid na Rafah, katika rasi ya Sinai ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Gazeti la al Yaum al Sab'i la Misri limeinukuu taarifa iliyotolewa jana (Jumatano) na jeshi la Misri ikisema kuwa, katika hatua ya pili ya oeresheni iliyopewa jina la "Haki ya Shahidi," mbali na kuuawa magaidi hao 85, jeshi la Misri limefanikiwa pia kuharibu maficho 190 na magari 10 ya magenge ya kigaidi.
Baadhi ya vyombo vya habari vilitangaza jana kuwa, wanamgambo 36 wameuawa katika mashambulizi yaliyofanyika katika mji wa Sheikh Zuweid pekee.
Katika wiki kadhaa zilizopita, askari wa Misri wamezidi kuyazingira maeneo ya makundi ya kigaidi kaskazini mwa nchi hiyo.
Tangu miezi kadhaa nyuma, jeshi la Misri lilianzisha operesheni kubwa katika maeneo ya Rafah, Sheikh Zuweid na al Aris huko Sinai Kaskazini kwa lengo la kuyamaliza magenge hayo ya kigaidi.