Wakazi wa Goma wapinga kupelekwa polisi wa Rwanda katika mji huo
Mamia ya wakazi wa mji wa Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamefanya maandamano kupinga kupelekwa askari polisi wa Rwanda katika mji huo.
Mapigano na ghasia zilishuhudiwa jana Jumatatu katika mji wa Goma, ambao ni makao makuu ya jimbo la Kivu Kaskazini, kati ya vijana waliokuwa na hasira wa Kongo na polisi wa nchi hiyo na kusababisha kujeruhiwa watu kadhaa na kuuliwa polisi mmoja. Vijana hao waliweka vizuizi barabarani ili kuwazuia polisi.
Mtu mmoja aliyeshiriki katika maandamano hayo amenukuliwa akisema kuwa, Kongo DR ina jeshi na polisi inayofaa lakini hawajui ni kwa nini polisi wa Rwanda wanataka kupelekwa nchini humo ili kudumisha amani.
Vijana hao waliokuwa na hasira wamefanya maandamano wakipinga uwepo wa polisi wa Rwanda katika mji wa Goma. Polisi wa Kongo wametumia gesi ya kutoa machozi na silaha hai kutawanya maandamano hayo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo Jumamosi iliyopita Kamishna Mkuu wa Polisi ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alikanusha madai kwamba polisi kutoka Rwanda wanatazamiwa kuwasili Goma na kuyataja madai hayo kuwa hayana msingi wowote.