Job Yustino Ndugai, Spika wa Bunge la Tanzania ajiuzulu
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai ametangaza kujiuzulu wadhifa wake huo ndani ya Bunge leo Alkhamisi, Januri 6, 2022.
Ndugai ametuma taarifa kwa vyombo vya habari ambayo Radio Tehran imepata taarifa hiyo ambayo sehemu yake moja inasema: "Naomba kutoa taarifa kwa umma wa Watanzania kuwa leo tarehe 06 Juanuri, 2022 nimeandika barua kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujiuzulu nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uamuazi huu ni binafsi na hiari na nimeufanya kwa kuzingatia na kujali maslahi mapana zaidi ya taifa langu, serikali na chama changu cha CCM."
Uamuzi huo wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umekuja kufuatia mvutano mkubwa wa kisiasa unaendelea nchini Tanzania hivi sasa kufuatia kauli yake aliyoitoa kuhusu Rais Samia Suluhu kukopa shilingi trilioni 1.3.
Katika sehemu nyingine ya taarifa yake kwa vyombo vya habari, Ndugai ametoa shukrani zake kwa Wabunge, kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa wananchi wa jimbo lake la Kongwa na Watanzania wote kwa ujumla kwa ushirikiano mkubwa waliompa katika kipindi chote alipokuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hapa chini tumeweka nakala ya taarifa yake hiyo kwa vyombo vya habari.
