Kwa nini India inashirikiana na utawala wa kizayuni wa Israel?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i129310
Katika miaka ya hivi karibuni India na utawala wa Kizayuni zimeanzisha uhusiano mkubwa katika sekta nyingi za kiuchumi, kijeshi na kisiasa.
(last modified 2025-08-09T02:29:20+00:00 )
Aug 09, 2025 02:29 UTC
  • Kwa nini India inashirikiana na utawala wa kizayuni wa Israel?

Katika miaka ya hivi karibuni India na utawala wa Kizayuni zimeanzisha uhusiano mkubwa katika sekta nyingi za kiuchumi, kijeshi na kisiasa.

Ukweli ni kwamba, miaka ya hivi karibuni imeshuhudia India ikijitenga na muelekeo wake wa muda mrefu katika eneo hilo ambao uliegemezwa kwenye misingi ya kuishi kwa amani na nchi za eneo hilo hususan majirani zake na imeanzisha uhusiano wenye matatizo na wa karibu kati yake na Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel. Tukitathimini hali hii tunaona hatari ya uingiliaji wa Marekani na Wazayuni katika masuala nyeti na muhimu ya kikanda katika Asia ya Magharibi.

Maafisa wa India wamechukua mtazamo tofauti katika miaka ya hivi karibuni, wakitaka kuimarisha mamlaka yao nje ya mipaka ya eneo la Asia Magharibi. Katika miaka ya hivi karibuni, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amefanya mikutano kadhaa na mwenzake wa Israel, Benjamin Netanyahu, na ameanzisha na kufikia makubaliano ya kina ya kijeshi na kibiashara na Tel Aviv.

Tangu kale hadi sasa, sera rasmi ya India kuhusiana na Palestina zimepitia mabadiliko makubwa. Utendaji wa viongozi wa India umebadilika kutoka kuwaunga mkono wananchi ambao wamekuwa wakiishi chini ya mabavu na uvamizi na kuwaunga mkono wavamizi. Himaya na uungaji mkono huo wa India haujaishia  tu kaika uga wa kisiasa na kiuchumi, lakini pia umefikia kiwango cha kijeshi.

 

Hii ni katika hali ambayo, mwaka 1947, India ilipiga kura katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ya kupinga kugawanywa Palestina na mnamo mwaka 1974 ilikuwa nchi ya kwanza isiyo ya Kiarabu kuitambua Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) kama "mwakilishi pekee halali wa watu wa Palestina".

Waaidha India ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza kabisa kulitambua taifa la Palestina. Hiyo ilikuwa mwaka 1988. Ingawa India iliutambua utawala wa Kizayuni mwaka 1950, lakini hadi kufikia mwaka 1993 haikuanzisha uhusiano wowote wa kidiplomasia na utawala huo ghasibu.

Uhusiano wa karibu na wa kushibana kati ya New Delhi na Tel Aviv unaweza kuonekana mwanzoni mwa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqswa Oktoba 7, 2023, ambapo, tofauti na siku za nyuma, maafisa wa India walikimbilia mara moja kutoa uungaji mkono mkubwa wa kisiasa kwa utawala wa Kizayuni mara tu baada ya operesheni hiyo iliyotekelezwa na wanamuqawama wa Palestina.

Saa chache tu baada ya operesheni hiyo, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza duniani kulaani operesheni hiyo. Subrahmanyam Jaishankar, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wan chi hiyo naye akafuata msimamo huo.

Wakati wa mvutano wa hivi majuzi kati ya India na Pakistan, tulishuhudia pia maafisa wa Israel wakiunga mkono rasmi mashambulizi ya India dhidi ya Pakistan na kulitafsiri hilo katika fremu ya haki ya kujilinda (suala ambalo wao wenyewe hutumia kuhalalisha uhalifu wa kivita dhidi ya Gaza).

Sambamba na uungaji mkono wake usio na masharti kwa utawala wa kizayuni wa Israel, serikali ya India ilijizuia kupiga kura ya kuunga mkono usitishaji mapigano huko Gaza katika Umoja wa Mataifa tarehe 27 Oktoba. Uungaji mkono huo wa kisiasa uliathiri msimamo wa Wahindu wenye misimamo mikali, ambao walianzisha kampeni kubwa kwenye mitandao ya kijamii kueneza habari za upotoshaji kuhusu Gaza kwa maslahi ya utawala wa kizayuni. Hatua hii ililenga kukuza propaganda za chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) na kuwalenga Waislamu walio wachache nchini India.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetoa waranti wa kukamaktwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na Waziri wa zamani wa Vita Yoav Gallant kwa kutenda jinai za kivita

 

Aidha katika miezi iliyofuata baada ya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqswa na Vita vya Gaza, licha ya jinai za kikatili za utawala wa Kizayuni zilizopelekea kufunguliwa mashtaka ya mauaji ya halaiki dhidi yake na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na hata kutolewa hati za kukamatwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na Waziri wa zamani wa Vita Yoav Gallant na Mahakama ya ICC kwa kutenda jinai za kivita, lakini serikali ya New Delhi iliruhusu baadhi ya mikusanyo ya kuunga mkono utawala wa kizayuni ifanyike nchini humo. Katika upande wa pili, serikali ya India ilikandamiza maandamano ya kuunga mkono Palestina na Gaza, hatua ambayo bila shaka iliweka wazi sera za India hivi sasa kuhusiana na kadhia ya Palestina.

Kwa muktadha huo, inaweza kusemwa kuwa, ukuruba kati ya India na utawala wa kizayuni wa Israel ni matokeo ya mchanganyiko wa mambo ya kiuchumi, kiusalama na mabadiliko ya sera za New Delhi. Ingawa uhusiano huu umekabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa baadhi ya makundi ya ndani na nje ya India, lakini inaonekana kuwa, kuna uwezekano wa kuendelea kwake katika siku zijazo.

Kuhusiana na suala hilo, uhusiano wa kisiasa, kibiashara, kidiplomasia na kijeshi kati ya India na utawala wa kizayuni umekuwa ukiongezeka tangu mwishoni mwa miaka ya 1990, na hatua kwa hatua pande hizo mbili zimekaribiana zaidi kutokana na baadhi ya matukio ya kieneo na kimataifa. Hata hivyo, licha ya azma kubwa ya viongozi wa New Delhi na Tel Aviv ya kukuza uhusiano wa pande mbili katika sekta nyingi, wananchi wa India pamoja na baadhi ya vyama vya siasa wakizingatia historia ya huko nyuma wamepinga misimamo ya viongozi wa nchi hiyo ya kuunga mkono Israel na kujifungamanisha na utawala huo vamizi na wameonyesha upinzani wao huo kwa nyakati tofauti na katika matukio mbalimbali.