Feb 07, 2016 13:54 UTC
  • EALA yataka kufanyika uchunguzi juu ya ukiukaji wa haki za binadamu Burundi

Bunge la Afrika Mashariki EALA limeelezea wasi wasi wake juu ya kukithiri visa vya ukiukaji wa haki za binadamu nchini Burundi na kutoa wito wa kufanyika uchunguzi huru kuhusu suala hilo.

Baada ya kuandaa kikao cha kusilikiza malalamiko kutoka kwa wananchi wa Burundi kuhusu hali ya kisiasa nchini humo, Kamati ya Masuala ya Kieneo na Utatuzi wa Migogoro ya bunge hilo la kieneo imesema kuwa kuna udharura wa kufanyika uchunguzi huru na wa kina juu ya ukiukaji wa haki za binadamu unaodaiwa kufanywa na vyombo vya usalama vya serikali ya Bujumbura. Abdullah Mwinyi, Mwenyekiti wa kamati hiyo amesema kuwa, pande zote zimekubali kuwa kuna wimbi la ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu nchini humo, ila zinatofautiana kuhusu waliohusika. Kwa msingi huo, kamati hiyo imelitaka Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki kwa idhini ya marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, liunge mkono pendekezo la kuundwa jopo huru la kuchunguza ukiukaji huo wa haki za binadamu Burundi.

Tangu Rais Pierre Nkurunziza alipotangaza nia ya kuwania urais kwa muhula wa tatu na kisha kushinda uchguzi huo, hali ya usalama imekuwa mbaya nchini Burundi na hadi sasa mamia ya watu wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa; huku maelfu wakilazimika kuikimbia nchi.

Tags