Mar 29, 2024 02:39 UTC
  • UN: Huenda Israel imetenda jinai ya kivita kwa kutumia njaa kama silaha ya vita

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema hatua ya utawala wa Israel kutumia njaa kama silaha dhidi ya watu Wapalestina wa Ukanda wa Gaza yumkini ikawa jinai ya kivita.

Volker Türk alisema hayo jana Alkhamisi katika mahojiano na shirika la utangazaji la BBC na kuongeza kuwa, ukubwa wa tatizo la kutengenezwa la chakula huko Gaza "haujawahi kutokea" katika historia ya karibuni.

Amesema kuna ushahidi ulioibuka kuwa Israel ama inachelewesha au inazuia kabisa ufikishaji wa chakula cha msaada kwa wakazi wa Gaza, na kwamba endapo madai hayo yatathibiti, basi Tel Aviv itakuwa imetenda jinai ya kivita. 

Kadhalika afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, upanuzi wa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina ni jinai ya kivita. Kwa mujibu wa azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina ni kinyume cha sheria.

Jinai za Israel Gaza

Umoja wa Mataifa umesema kuwa watoto wote walio chini ya umri wa miaka mitano huko Gaza wanakabiliwa na utapiamlo na wako katika hatari ya uharibifu usioweza kurekebishwa katika ukuaji wao wa kimwili na kiakili.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN ameongeza kuwa, utawala wa Israel unatumia njaa kama silaha dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza ambao wanakabiliwa na mgogoro mkubwa wa chakula baada ya miaka ya vikwazo na mzingiro.

Mgogoro wa chakula huko Gaza unakuja huku kukiwa na ongezeko kubwa la mauaji yanayofanywa na Israel, ambapo utawala huo pandikizi mpaka sasa umewaua shahidi Wapalestina zaidi ya 32,400 katika kipindi cha miezi sita iliiyopita.

Tags