Umoja wa Mataifa wataka kufanyika mazungumzo mapana Burundi
Umoja wa Mataifa umetaka yafanyike mazungumzo mapana kati ya wapinzani na serikali ya Burundi.
Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa jana alizitolea wito pande husika katika mgogoro wa Burundi kufanya mazungumzo mapana na kukaribisha uamuzi wa msuluhishi wa kieneo wa kufanya mazungumzo na wapinzani wa nchi hiyo.
Ban Ki-moon pia amepongeza juhudi za Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin William Mkapa za kufanikisha kufanyika mazungumzo ya amani kati ya pande zinazozozana Burundi mnamo tarehe 21 na 24 mwezi huu huko Arusha Tanzania. Aidha Mkapa amesema amepanga kukutana na kufanya mazungumzo na makundi muhimu ya wapinzani wa Burundi wiki mbili zijazo. Itakumbukwa kuwa makundi hayo yalikataa kushiriki kwenye mazungumzo ya Arusha Tanzania. Hatua ya Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi ya kuwania urais kwa muhula wa tatu ambako kwa mujibu wa wapinzani ni kinyume na katiba, kumeitumbukiza nchi hiyo kwenye mgogoro wa kisiasa tangu mwanzoni mwezi Aprili mwaka jana.