Watu 60 wauawa katika shambulio la wabeba silaha DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i79912-watu_60_wauawa_katika_shambulio_la_wabeba_silaha_drc
Kwa akali watu 60 wameuawa katika shambulio la kundi moja la wabeba silaha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 02, 2022 22:58 UTC
  • Watu 60 wauawa katika shambulio la wabeba silaha DRC

Kwa akali watu 60 wameuawa katika shambulio la kundi moja la wabeba silaha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Duru za habari zimeliambia shirika la habari la Reuters kuwa, wanamgambo hao wa CODECO walilenga kambi ya wakimbizi wa ndani ya Savo katika mkoa wa Ituri, mapema jana Jumatano na kutekeleza ukatili huo.

Charite Banza Bavi, rais wa kundi moja la kiraia katika eneo la Bahema kaskazini mwa mkoa huo amesema idadi ya watu waliouawa katika kambi hiyo yenye wakimbizi 4,000 ni watu 63.

Serikali ya DRC haijatoa taarifa yoyote kuhusu shambulio hilo la kuogofya dhidi ya kambi ya wakimbizi wa ndani mkoani Ituri, mashariki mwa nchi.

Ramani inayoonesha mkoa wa Ituri wa kaskazini mashariki mwa DRC

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, waasi wa CODECO wanaojumuisha wapiganaji ambao wanadai kutetea haki za jamii ya wakulima Walendu dhidi ya wafugaji wa jamii ya Hema, wameuawa mamia ya watu, na kuwalazimisha maelfu ya wengine kuyakimbia makazi yao katika mkoa wa Ituri katika miaka ya hivi karibuni.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, wanajeshi wasiopungua 33 waliuawa katika mapigano yaliyozuka baina ya wanajeshi wa serikali na waasi wa M23 kaskazini mashariki mwa Kongo DR.