Apr 12, 2022 02:41 UTC
  • Cyril Ramaphosa
    Cyril Ramaphosa

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema ni jambo la kusikitisha kuona kuwa hisia na hujuma dhidi ya raia wa kigeni zinashabihiana na yale yaliyokuwa yakijiri nchini humo katika zama za utawala wa ubaguzi wa rangi au apathaidi.

Wiki iliyopita wakazi wa mji wa Diepsloot walifanya maandamano makubwa kupinga kuwepo raia wa kigeni eneo hilo.

Hivi karibuni pia raia wa Zimbabwe, Elvis Nyathi, aliuawa wakati magenge ya vijana walipokuwa wakienda nyumba hadi nyumba kuwatimua watu wasio raia wa Afrika Kusini.

Katika hotuba yake ya kila wiki Jumatatu ya jana, Ramaphosa alisema magenge yanayopinga raia wa kigeni ni sawa na madhalimu wa zama za utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo.

Aidha amekiri kuwa wananchi wengi wanakosoa kikosi cha polisi ambacho kimeshindwa kukabiliana na wahalifu. Amesema serikali yake ina mpango wa kuajiri maafisa wengine 12 elfu wa polisi ili kukabiliana na wahalifu.

Hujuma dhidi ya raia wa kigeni Afrika Kusini

Ramaphosa amesema wahalifu ndio maadui na si raia wa kigeni waliohamia nchini humo. Umaskini umetajwa kuwa  chanzo kikuu cha mvutano baina ya raia wa Afrika Kusini na raia wa kigeni.

Hii si mara ya kwanza kushuhudia ongezeko la chuki dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini. Mwaka 2008 kuliibuka wimbi la mashambulizi nchini kote dhidi ya wakimbizi na wahamiaji, na zaidi ya watu 60 waliripotiwa kuuawa na maelfu kuyahama makazi yao. Mwaka 2015 pia kuliripotiwa ghasia zaidi dhidi ya watu wasiokuwa Waafrika Kusini, hasa katika miji ya Durban na Johannesburg, ambayo ilisababisha kutumwa jeshi ili kuzuia machafuko zaidi.

Miaka mitatu iliyopita pia ongezeko jingine la mashambulizi dhidi ya wageni lilisababisha mamia ya Wanigeria kuondoka Afrika Kusini.

Tags