Apr 25, 2022 10:40 UTC
  • Watu 160 wauawa katika mapigano mapya Darfur, Sudan

Watu wasiopungua 160 wameuawa katika jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan baada ya kuibuka mapigano baina ya makundi mawili hasimu.

Hayo yalisemwa jana Jumapili na Adam Rigal, Msemaji wa Kamati Kuu ya Wakimbizi wa Darfur ambaye amefafanua kuwa, mbali na vijiji kadhaa kuchomwa moto, watu zaidi ya 45 wamejeruhiwa katika mapigano hayo ya kikabila katika mkoa wa Darfur Magharibi nchini Sudan.

Kiongozi mmoja wa kabila la jamii ya watu wachache la Massalit amenukuliwa na vyombo vya habari akisema maiti zimetapakaa katika vijiji vya eneo la Krink, yapata kilomita 80 kutoka mji wa Geneina, makao makuu ya mkoa wa Darfur Magharibi. Mauaji hayo yametokea wiki chache baada ya kuripotiwa mauaji mengine kama hayo katika jimbo hilo.

Mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, mapigano mengine makali kati ya makundi hasimu huko Darfur yalisababisha watu 45 kuuawa, huku viongozi wa kikabila wakiripoti kwamba mapigano hayo ni sehemu ya ghasia za kikabila zinazoendelea katika eneo hilo.

Ramani ya Sudan inayoonesha eneo la Darfur

Mzozo wa kugombania ardhi baina ya makabila ya Waarabu na wasio Waarabu katika eneo lenye milima mingi la Jebel Moon mkoa wa Darfur Magharibi umesababisha mapigano ya umwagaji damu na mauaji ya mamia ya watu tokea Novemba mwaka jana hadi sasa.

Eneo la Darfur mwaka 2003 lilikumbwa na mapigano ya umwagaji damu kati ya serikali ya wakati huo ya Sudan chini ya uongozi wa Rais aliyeondolewa  madarakani, Omar Hassan al-Bashir, na wapinzani wa serikali.

Malaki ya watu waliuawa na mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi katika mashambulizi hayo; na tokea wakati huo, eneo hilo limekuwa uwanja wa mapigano na umwagaji damu.

Tags