Idadi ya wahanga wa mripuko wa Mogadishu yafikia 15
Idadi ya watu waliofariki dunia katika mripuko wa bomu uliotokea hapo jana katika hoteli moja mjini Mogadishu, mji mkuu wa Somalia imeongezeka na kufikia watu 15.
Hayo yamethibitishwa na kamanda wa polisi nchini Somalia, Ibrahim Hassan ambaye ameongeza kuwa watu wengine 20 wamejeruhiwa vibaya. Jana kundi la kigaidi na kitakfiri la ash-Shabab lilishambulia hoteli hiyo kwa gari iliyokuwa imetegwa ndani yake mada za miripuko sanjari na kuwafyatulia risasi watu waliokuwepo hotilini hapo. Kamanda Hassan ameongeza kuwa, katika hujuma hiyo shakhsia kadhaa wakiwamo wawakilishi wa bunge la nchi hiyo waliokolewa salama. Licha ya wanachama wa kundi hilo kufurushwa na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika AMISOM kutoka mjini Mogadishu hapo mwaka 2011, lakini wamekuwa wakitekeleza hujuma za kigaidi katika maeneo tofauti ya mji huo. Kundi hilo linatekeleza hujuma na mashambulizi yake nchini Somalia kwa lengo la kuing'oa serikali madarakani ambapo wanachana wake hushambulia viongozi wa serikali, askari, ofisi na hata mahoteli wanamoishi viongozi wa serikali hiyo.