Watu 20 wauawa katika shambulizi la ADF mashariki ya DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i84472-watu_20_wauawa_katika_shambulizi_la_adf_mashariki_ya_drc
Makumi ya watu wameuawa katika shambulizi jipya la waasi wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) katika mkoa wa Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 07, 2022 03:38 UTC
  • Watu 20 wauawa katika shambulizi la ADF mashariki ya DRC

Makumi ya watu wameuawa katika shambulizi jipya la waasi wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF) katika mkoa wa Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa mujibu wa shirika la kiraia la Kivu Security Tracker (KST), watu wasiopungua 20 wameuawa baada ya wabeba silaha wanaoaminika kuwa wanachama wa ADF kushambulia kijiji cha Bwanasura katika eneo la Irumu mkoani Ituri.

Hata hivyo Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu katika eneo la Irimu, David Beiza, amesema "nimehesabu miili 36 katika eneo la mauaji ya halaiki."

Jana Jumatatu pia, waasi wa M23 walishambulia kwa mabomu ngome ya jeshi la DRC katika kijiji cha Bugusa eneo la Rutshuru mkoani Kivu Kaskazini, na kuua wanajeshi wawili na kujeruhi wengine watano.

Vikosi vya Jeshi la Uganda (UPDF) na  Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) vilianzisha mashambulizi mwaka jana ili kuwaondoa waasi hao wa ADF, ambao wamekuwa wakiwashambulia na kuwaua raia mashariki kwa zaidi ya miongo miwili.

Waasi wa ADF

Lakini licha ya operesheni za pamoja na hali ya kuzingirwa iliyotangazwa katika majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini kusitisha ghasia, waasi hao wangali wanaendelea kufanya mashambulizi. Wiki iliyopita, Uganda na DRC zilitangaza kuongeza muda wa operesheni ya pamoja ya kijeshi iliyoanzishwa mwishoni mwa mwaka jana dhidi ya waasi wa ADF mashariki mwa Congo

Kundi hilo la waasi linalotokea kaskazini mashariki mwa Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa DRC tangu muongo wa 90, ambapo limeua mamia ya watu, na kupelekea malaki ya wengine kuwa wakimbizi.