Tunisia: Hatufanyi mazungumzo ya kidiplomasia na Israel
Tunisia imekadhibisha ripoti ya baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuwa imeanzisha mazungumzo ya kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Katika taarifa jana Alkhamisi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Tunisia imesema hatua ya tovuti za habari zenye mfungamano na Israel kueneza uvumi huo usio na msingi wowote inakusudia kuchafua jina na sura ya taifa hilo la Kiarabu la kaskazini mwa Afrika.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa, Tunisia haina nia ya kuanzisha uhusiano wowote wa kidiplomasia na utawala unaozikaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina, na daima itaendelea kuwaunga mkono Wapalestina katika mapambano yao, hadi pale watakaporejeshewa haki zao za halali.
Juzi Jumatano, baadhi ya vyombo vya habari vya Waarabu vikinukuu tovuti ya Kizayuni ya Hayom vilitangaza habari za uvumi kuwa, kuna mazugumzo yanaendelea baina ya Israel na Tunisia juu ya uwezekano wa kuanzisha uhusiano wa kawaida baina ya pande mbili hizo.
Itakumbukwa kuwa, Aprili mwaka huu, Kituo cha Taifa cha Mawakili nchini Tunisia kiliwataka viongozi wa nchi hiyo kupasisha sheria ya kulitambua suala la kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel kuwa ni jinai na uhalifu.
Nchi nne za Kiarabu za Imarati (UAE), Bahrain, Morocco na Sudan mwaka 2020 zilisaini hati za makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni, hatua ambayo imeendelea kupingwa na kulaaniwa vikali katika nchi za Kiarabu na Kiislamu.
Wananchi waliowengi katika nchi hizo wanasema kuwa, hatua hiyo ni khiyana na usaliti mkubwa kwa wananchi wa Palestina wanaofanyiwa unyama wa kila aina na utawala wa Israel kila uchao.