DRC yafunga mpaka na Rwanda baada ya askari wake kuuawa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza kufunga mpaka wake na Rwanda baada ya askari wa jeshi la DRC kuuawa kwa kupigwa risasi wakati jeshi hilo lilipowashambulia askari wanaolinda mpaka ndani ya ardhi ya Rwanda.
Tukio hilo lililofanyika jana Ijumaa karibu na mji wa Goma wa mashariki mwa DRC, limeshadidisha taharuki na uwezekano wa mataifa hayo mawili jirani kuvunja uhusiano wao wa kidiplomasia.
Ofisi ya Gavana wa Kivu Kusini imetangaza kuwa, mpaka wa DRC na Rwanda ulifungwa kuanzia saa tisa mchana jana Ijumaa, huku serikali ya Kinshasa ikisema inachunguza tukio hilo.
Jeshi la Ulinzi la Rwanda limesema katika taarifa kuwa, askari wa DRC alivuka mpaka na kuingia ndani ya ardhi ya nchi hiyo, na kushambulia kwa risasi kituo cha upekuzi cha Rubavu, ambapo watu kadhaa walijeruhiwa.
Taarifa hiyo imesema askari huyo wa Kongo DR aliuawa na askari wa mpakani wa Rwanda kwa kupigwa risasi mita 25 ndani ya ardhi ya Rwanda. Jeshi la DRC wiki iliyopita pia lilidai kuwa Rwanda imetuma mamia ya askari ndani ya ardhi ya nchi hiyo, huku wasiwasi na taharuki ikiendelea kushuhudiwa kati ya nchi hizo jirani na kutishia uhusiano baina yao.
Haya yanajiri siku chache baada ya DRC kusitisha mikataba yote iliyotiliana saini na jirani yake Rwanda baada ya kuongezeka mzozo na mvutano baina ya mataifa haya mawili jirani.
Mgogoro wa kidiplomasia baina ya Kigali na Kinshasa umeongezeka katika siku za hivi karibuni baada ya pande zote mbili kutuhumiana kuwa zinaunga mkono waasi mashariki mwa eneo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo linalopakana na Rwanda.