Uchaguzi wa Bunge Somalia kufanyika Agosti
Bunge jipya la Somalia litaundwa Agosti mwaka huu ambapo rais na viongozi wa majimbo watakutana Juni 20 kujadili njia za kuwateua wabunge hao kwani hawachaguliwi kwa kura ya moja kwa moja ya wananchi.
Ofisi ya rais wa Somalia imetoa taarifa na kusema kongamano hilo kuhusu kuwachagua wabunge litafanyika mjini Baidoa katika muda uliopangwa na wala muhula wa bunge la sasa hautaongezwa.
Katika uchaguzi wa mwaka 2012, wabunge wa Somalia walichaguliwa na jopo la wazee na kisha wabunge hao wakamchagua Hassan Sheikh Mohamud kuwa rais wa Somalia.
Huo ulikuwa upigaji kura wa kwanza tokea mwaka 1991 wakati mababe wa kivita walipomuondoa madarakani Rais Mohammad Siad Barre na kuitumbukiza nchi hiyo katika vita.
Uchaguzi huo ni muhimu kwa Somalia ambayo inakabiliana na hujuma za kundi la kigaidi la Al Shabab linalotaka kuipindua serikali ya nchi hiyo.