Walipiza Kisasi wa Delta, Nigeria: Msishambulie askari wala kuteka nyara raia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8527-walipiza_kisasi_wa_delta_nigeria_msishambulie_askari_wala_kuteka_nyara_raia
Kundi la wanamgambo linalojiita Walipiza Kisasi wa Niger Delta nchini Nigeria limeyataka makundi mengine ya wanamgambo nchini humo kutoshambulia askari wala kuteka nyara raia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 05, 2016 10:56 UTC
  • Walipiza Kisasi wa Delta, Nigeria: Msishambulie askari wala kuteka nyara raia

Kundi la wanamgambo linalojiita Walipiza Kisasi wa Niger Delta nchini Nigeria limeyataka makundi mengine ya wanamgambo nchini humo kutoshambulia askari wala kuteka nyara raia.

Kundi hilo ambalo limetangaza kuhusika na mashambulio kadhaa dhidi ya miundombinu ya mafuta limetoa wito huo likisisitiza kuwa katika mashambulio yake liliyofanya halijaua hata mtu mmoja.

Kundi la Walipiza Kisasi wa Niger Delta aidha limelitaka kundi jengine la wanamgambo ambalo limesema lina makombora ya kutungulia ndege kutotumia makombora hayo kuilenga ndege yoyote.

Taarifa iliyotolewa na kundi hilo imesisitiza kuwa "vita vinalenga mitambo ya mafuta" na kuashiria makundi mapya yanayoibuka kila siku na kutanabahisha kuwa kundi hilo litakabiliana na kundi lolote litakalokataa wito huo na kuwashambulia wanajeshi.

Kundi la Walipiza Kisasi wa Niger Delta limetoa wito huo kwa wale liliowaita ndugu zake katika mapambano katika maeneo ya Rivers, Ondo, Delta, Bayelsa, Cross River na Akwa Ibom kutojihusisha na kitendo chochote cha utekaji nyara na kushambulia askari.

Wimbi la karibuni la mashambulio katika eneo la Niger Delta ambalo ndicho kitovu cha uzalishaji mafuta ya Nigeria limesababisha kupungua uzalishaji wa mafuta ya nchi hiyo na kufikia kiwango cha chini zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Harakati za uasi katika eneo la Niger Delta zimegawika katika makundi kadhaa, kila moja likiwa na madai yake.

Makundi hayo yametangaza kuwa lengo lao ni kuhakikisha yanasimamisha kikamilifu uzalishaji mafuta wa nchi hiyo ambao kwa mujibu wa Waziri wake wa mafuta, hivi sasa umefikia mapipa milioni 1.6 kwa siku kutoka mapipa milioni mbili kwa siku wakati ulipoanza mwaka huu wa 2016.../