Burundi hali bado si shwari
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8629-burundi_hali_bado_si_shwari
Anga ya kisiasa nchini Burundi imeendelea kuwa mbaya, huku duru za habari zikiripoti habari ya kutiwa nguvuni na maafisa usalama wa nchi hiyo mwandishi wa habari Egide Ndayisenga.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 06, 2016 09:44 UTC
  • Burundi hali bado si shwari

Anga ya kisiasa nchini Burundi imeendelea kuwa mbaya, huku duru za habari zikiripoti habari ya kutiwa nguvuni na maafisa usalama wa nchi hiyo mwandishi wa habari Egide Ndayisenga.

Kwa mujibu wa habari hiyo, Ndayisenga alikamatwa hivi karibuni katika eneo la Cibitoke jambo ambalo limeongeza hali ya wasi wasi miongoni mwa raia wa nchi hiyo. Egide Ndayisenga ametiwa mbaroni kwa tuhuma za kuwa na mahusiano na makundi ya upinzani ya nchini Rwanda. Kabla ya hapo, Alain Guillaume Bunyoni, Waziri wa Usalama wa Jamii nchini Burundi alikuwa ametaka kutiwa mbaroni waandishi wa habari wenye kukabiliwa na tuhuma za kufanya jinai na kusababisha machafuko nchini humo. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, tangu mwaka jana jumla ya waandishi wa habari wapatao 100 wamekimbia nchi hiyo, wengi wao wakitia kambi nchi jirani ya Rwanda. Hayo yanajiri katika hali ambayo kwa muda mrefu sasa serikali ya Bujumbura imekuwa ikimlaumu jirani yake huyo 'Rwanda' kwa kile inachosema kuwa ni hatua ya Kigali ya kuwaunga mkono waasi wanaotaka kumuondoa madarakani Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo.