Upinzani DRC wakosoa vikali mikakati ya Rais Tshisekedi ya kukabiliana na Rwanda
(last modified Sun, 07 Aug 2022 02:59:00 GMT )
Aug 07, 2022 02:59 UTC
  • Upinzani DRC wakosoa vikali mikakati ya Rais Tshisekedi ya kukabiliana na Rwanda

Wapinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamemlaumu vikali Rais Felix Tshisekedi na mikakati yake ya kuamiliana na Rwanda kufuatia ripoti iliyotolewa hivi karibuni na wataalamu wa Umoja wa Mataifa inayoeleza kwamba serikali ya Kigali imekuwa ikilisaidia na kuliunga mkono kundi la waasi wa M23 linalopigana na serikali ya Kinshasa.

Wanasiasa kwa ujumla na hasa kambi ya upinzani imetaka yafanyike mabadiliko katika mikakati ya serikali.

Mbunge Juvénal Munubo, ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge la Taifa amesema, kufuatia ripoti iliyotolewa na wataalamu wa UN serikali ya DRC serikali, inapaswa kuwasilisha malalamiko yake mbele ya vyombo vya sheria vya kimataifa.

Kwa mujibu Munubo, katika ngazi ya kidiplomasia, kuna umuhimu kwa serikali ya rais Tshisekedi kutathmini upya utekelezwaji wa ramani ya mchakato ulioafikiwa mjini Luanda, Angola, kati ya Kigali na Kinshasa.

Katibu Mkuu wa chama cha UNC, Billy Kambale ameyaelekezea kidole cha tuhuma madola makubwa akisema: "tunahisi DRC inaumizwa na mataifa makubwa. Na wanaruhusu nchi jirani kufanya shughuli zao katika ardhi yetu (…) ili kuyumbisha usalama wa nchi yetu. Jumuiya ya kimataifa lazima pia itusaidie kukomesha vitendo hivi vya makundi yenye silaha yanayoungwa mkono na nchi jirani. "

Rais Felix Tshisekedi wa DRC

Martin Fayulu, aliyewahi kuwania kiti cha urais, ameishutumu serikali kwa "kupotoshwa" na akasisitiza kuwa anatarajia itachukua hatua madhubuti kama ya kumfukuza mara moja balozi wa Rwanda aliyeko Kinshasa. Aidha ametilia mkazo udharura wa kulifanyia mageuzi jeshi la DRC na kulipatia uwezo zaidi.

Msimamo huo wa Fayulu umeungwa mkono na mbunge wa chama chake cha Ecidé,  Jean-Baptiste Kasekwa, ambaye pia ni naibu katibu mkuu wa chama hicho ambaye amesema: "tunasubiri kufukuzwa balozi wa Rwanda nchini DRC na tunasubiri kuvunjwa uhusiano wa kidiplomasia hadi Rwanda itakaporejea kwenye hisia nzuri na kukubali kuheshimu uhuru na uadilifu wa taifa la DRC. (…) Tunataka hatua kali, amesisitiza mbunge huyo.../

 

Tags