Maiti 20 za wahajiri zapatikana katika mpaka wa Libya na Sudan
(last modified Sat, 13 Aug 2022 11:24:02 GMT )
Aug 13, 2022 11:24 UTC
  • Maiti 20 za wahajiri zapatikana katika mpaka wa Libya na Sudan

Maiti 20 za wahajiri haramu zimepatikana katika jangwa lililoko baina ya Libya na Sudan.

Taarifa iliyotolea na Vikosi vya Pamoja vya Libya na Sudan imesema, miili hiyo ya wahajiri haramu imepatikana katika mipaka ya eneo la Darfur Kaskazini na Libya.

Taarifa hiyo iliyonukuliwa na shirika rasmi la habari la Sudan SUNA imeeleza kuwa, wahajiri wanane wamepatikana wakiwa hai kwenye msako uliofanywa na wanajeshi wa vikosi hivyo vya pamoja.

Habari zaidi zinasema kuwa, wahajiri hao walikuwa wakisafiri kwa magari mawili kwenda Libya wakitokea nchi jirani ya Sudan kabla ya kukwama kwenye jangwa hilo. Haijabainika iwapo magari waliokuwa wakisafiria yaliharibika au yalishambuliwa.

Taarifa ya Vikosi vya Pamoja vya Libya na Sudan ingawaje haitaeleza kuhusu uraia wa wahajiri walioaga dunia katika mazingira ya kutatanisha kwenye mkasa huo, lakini imeeleza kuwa wahajiri wanane waliookolewa ni raia wa Sudan.

Maiti zilivyopatikana jangwani

Kanali Ali Said, Kamanda wa vikosi hivyo amesema, askari wa nchi mbili hizo jirani wanashirikiana kuimarisha usalama mipakani na kukabiliana na wahajiri haramu na watu wanaofanya magendo ya binadamu.

Mamlaka za Sudan zimesema zimeimarisha operesheni za kukabiliana na magenge yanayofanya magendo ya binadamu na kuwasafirisha wahajiri kinyume cha sheria kuelekea Ulaya kupitia Libya.