Oct 06, 2022 13:43 UTC
  • NGOs zakosoa mradi wa mafuta wa Uganda

Ripoti iliyotolewa na taasisi mbili za kulinda mazingira zisizo za kiserikali imetahadharisha kuhusu uwezekano wa kujitokeza uharibifu na taathira za kimazingira kutokana na mradi wenye utata unaohusisha kampuni kubwa ya mafuta ya Ufaransa ya TotalEnergies na Shirika la Kitaifa la Mafuta la Offshore la China (CNOOC).

Kampuni mbili hizo mapema mwaka huu zilisaini makubaliano ya dola bilioni 10 kuendeleza visima vya mafuta vya Uganda na kusafirisha mafuta ghafi kupitia bomba la mafuta lenye kilomita 1,445 hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania katika pwani ya Bahari ya Hindi.   

Ripoti hiyo imeeleza kuwa, bomba hilo litatoa hadi tani milioni 34 za hewa ya kaboni kwa mwaka hewani; kiwango ambacho kimetajwa kuwa ni zaidi ya uzalishaji wa gesi chafu kwa pamoja nchini Uganda na Tanzania".

Mradi mkubwa wa visima vya mafuta wa Uganda 

Taasisi hizo za kulinda mazingira zisizo za kiserikali zimezituhumu kampuni hizo za mafuta kwa kutochukua hatua za kutosha za kuzilinda jamii na mazingira kwa ujumla. 

Wakati huo huo kampuni ya TotalEnergies imetoa radiamali yake kwa ripoti hiyo ikisema kuwa, itafanya kila linalowezekana ili mradi huo uwe mfano wa kuigwa katika suala la uwazi, ustawi wa pamoja, maendeleo ya kiuchumi na kijamii, maendeleo endelevu, kulinda mazingira na kuheshimu haki za binadamu”.

Tayari Bunge la Ulaya limepasisha azimio likisema kuwa zaidi ya watu laki moja wako katika hatari ya kuhama makazi yao kufuatia mradi huo wa bomba la mafuta na kutaka watu hao walipwe fidia ya kutosha. 

Tags