Mafuriko yaua watu 24 kaskazini mwa Nigeria
(last modified Sat, 08 Oct 2022 11:12:43 GMT )
Oct 08, 2022 11:12 UTC
  • Mafuriko yaua watu 24 kaskazini mwa Nigeria

Watu wasiopungua 24 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha katika jimbo la Katsina la kaskazini mwa Nigeria.

Hayo yamesemwa na Umar Muhammad, Mkuu wa Idara ya Kusimamia Hali za Dharura ya jimbo la Katsina ambaye ameeleza kuwa, mafuruki hayo yamewalazimisha watu 18,000 kuyahama makazi yao.

Ameongeza kuwa, mafuruko hayo yamesomba nyumba 16,625 katika mitaa 34 ya jimbo hilo, huku ekari 1,620 za mashamba ya kilimo zikiharibiwa na maji ya mafuriko hayo tangu msimu wa mvua uanze mwezi Mei.

Duru za habari zinaarifu kuwa, sehemu kubwa ya ardhi na maeneo ya makazi ya watu katika jimbo hilo yamefunikwa na maji ya mafuriko kutokana na mifumo mibovu ya njia za maji. 

Ramani ya Nigeria inayoonesha jimbo la Katsina

Mvua kubwa zilizosababisha mafuriko zimefanya uharibifu mkubwa wa mali na roho za watu kaskazini mwa Nigeria. Watu wasiopungua 50 wamefariki dunia katika jimbo la Jigawa kaskazini mwa nchi tangu mwishoni mwa mwezi Julai.

Idara ya Hali ya Hewa ya Nigeria imetahadharisha pia kuhusu mvua kali zitakazonyesha siku zijazo katika mikoa kadhaa ya kaskazini mwa nchi hiyo kama vile Jigawa, Kano, Borno, Kaduna, Bauchi, Yobe na Katsina.