Jun 11, 2016 04:18 UTC
  • Uganda kuondoa askari wake wanaowasaka waasi wa LRA, nchini CAR

Uganda imesema karibuni hivi itawaondoa askari wake wanaoongoza katika operesheni ya kuwasaka waasi wa Lord's Resistance Army (LRA) katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Paddy Ankunda, msemaji wa jeshi la Uganda pasina kutoa sababu zozote alisema jana Ijumaa kuwa, kufikia mwishoni mwa mwaka huu, serikali ya Kampala itawaondoa askari wake katika kikosi cha askari wa Afrika kinachowasaka waasi wa LRA katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Hata hivyo azma hiyo ya Uganda tayari imekabiliwa na pingamizi kutoka Umoja wa Afrika, ambao unaitaka kutoondoa askari hao mara moja bali isubiri kidogo. Msemaji wa jeshi la Uganda amesema UPDF kwa sasa inatathmini ombi hilo la AU kujua iwapo italizingatia au la.

Hivi sasa kikosi cha askari 3,000 wa Afrika kinachoongozwa na Uganda kinawasaka waasi wa LRA akiwemo kiongozi wao Joseph Kony. Kikosi hicho kinajumuisha pia askari wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kundi la waasi wa Kikristo la LRA liliasisiwa kaskazini mwa Uganda kwa shabaha ya kuasisi utawala nchini humo uliosimama juu ya amri kumi za Biblia.

Waasi hao walipanua wigo wa harakati zao na kuvuka mpaka ambapo waliingia mashariki mwa Kongo na baadaye katika ardhi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Tags