Oct 16, 2022 11:19 UTC
  • Uganda yafunga wilaya 2 ili kudhibiti msambao wa Ebola

Serikali ya Uganda imetangaza habari ya kuziweka wilaya mbili za nchi hiyo katika karantini, kwa lengo la kudhibiti mripuko wa virusi vya Ebola unaoshuhudia katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwa wiki kadhaa sasa.

Katika utekelezaji wa karantini hiyo, mabaa, maabadi, na kumbi za starehe zitafungwa kwa wiki tatu katika wilaya za Mubende na Kassanda, katikati mwa nchi.

Mripuko wa hivi sasa ulianzia katika wilaya ya Mubende katikati mwa Uganda, karibu kilomita 150 magharibi mwa mji mkuu Kampala, kabla ya kuenea katika wilaya jirani ya Kassanda.

Wilaya hizo zimewekewa vizuizi katika hali ambayo, mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda alisema nchi hiyo haitatangaza hatua za karantini katika hatua za kudhibiti mripuko wa ugonjwa hatari wa Ebola ncini humo.

Alisema kuwa hapana haja ya kuweka vizuizi kwa sababu ameona pana urahisi kudhibiti maambukizi ya Ebola ikilinganishwa na maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19.

Hata hivyo kutangazwa kwa karantini katika wilaya hizo ambazo ni kitovu cha mripuko wa sasa, kunaashiria kuenea kwa kasi kwa maambukizo ya maradhi hayo.  

Haya yanajiri huku idadi ya watu walioaga dunia nchini Uganda kwa maradhi hatari ya Ebola ikiongezeka na kufikia 19, miongoni mwa kesi 58 zilizonakiliwa. Hayo ni kwa mujibu wa takwimu rasmi za serikali. Hata hivyo vyanzo huru vinasema idadi ya walipoteza maisha kwa maradhi hayo wanakaribia 30.  

Tags