Morocco yazuia wahajiri 56,000 kwenda Ulaya kupitia Mediterania
Mamlaka za Morocco zimetangaza kuwa zimezima majaribio ya makumi ya maelfu ya wahamiaji haramu waliojaribu kuvuka bahari ya Mediterania kuelekea Ulaya.
Ripoti iliyotolewa na Bunge la Morocco imesema kuwa, vyombo vya dola nchini humo vimezuia wahajiri 56,000 kwenda Ulaya kupitia Mediterania kati ya Januari na Agosti mwaka huu.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa, wahajiri haramu 12,000 ambao nusra wafe maji katika bahari ya Mediterania waliokolewa na mabaharia na askari wa Gadi ya Pwani ya Morocco katika kipindi hicho cha miezi minane ya kwanza ya mwaka huu.
Kunafanyika majaribio mengi ya kuvuka bahari ya Mediterania hasa wakati wa majira ya joto. Maelfu ya wahajiri hao haswa Kiafrika huaga dunia kila mwaka katika safari hizo za kuogofya wakitumia mitumbwi dhaifu na boti za plastiki.
Juni mwaka huu, Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika alilaani mauaji ya makumi ya wahajiri wa Kiafrika katika mpaka wa Morocco na Uhispania. Wahajiri karibu 30 waliaga dunia katika mkanyagano wa kujaribu kuvuka uzio na kuingia katika maeneo ya Melilla na Ceuta yanayodhibitiwa na Uhispania.
Mwaka 2020, serikali ya Morocco ilisema imezua wahamiaji haramu 12,231 kuingia Ulaya kupitia safari hizo hatarishi za baharini na vile vile kupitia mipaka ya ardhini ya Melilla na Ceuta.
Kutokana na kuwa kwao kaskazini mwa Afrika, Morocco, Tunisia na Libya ni vituo maarufu vya kupita wahamiaji haramu kwenda Ulaya kwa ndoto za kupata maisha bora.