Makumi wauawa katika mapigano makali jijini Bujumbura
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9061-makumi_wauawa_katika_mapigano_makali_jijini_bujumbura
Duru za habari nchini Burundi zimeripoti kujiri mapigano makali kati ya askari wa serikali na waasi katika maeneo kadhaa ya jiji la Bujumbura, mji mkuu wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 12, 2016 09:51 UTC
  • Makumi wauawa katika mapigano makali jijini Bujumbura

Duru za habari nchini Burundi zimeripoti kujiri mapigano makali kati ya askari wa serikali na waasi katika maeneo kadhaa ya jiji la Bujumbura, mji mkuu wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa duru hizo, makumi ya watu wameuawa kati ya pande mbili katika mapigano hayo yaliyojiri jana usiku. Redio ya serikali imetangaza mchana wa leo kuwa, karibu waasi 20 wameuawa katika mapigano hayo huku askari wawili wakiwa ni miongoni mwa waliopoteza maisha. Aidha taarifa hiyo ya redio ya serikali imeongeza kuwa katika mapigano hayo yaliyojiri katika eneo la Buyenzi, Kinama, Cibitoke, Musaga na Ngangara yamepelekea watu kadhaa kujeruhiwa baadhi yao wakiwa katika hali mahututi. Hii ni katika hali ambayo baadhi ya duru zisizo za kiserikali zimearifu kuuawa askari 24 wa serikali huku makumi ya wengine wakijeruhiwa. Watu walioshuhudia wamewataja waasi hao waliohusika na hujuma hiyo kuwa ni kundi la 'Red Tabara' ambao wanapinga uongozi wa muhula wa tatu wa Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo. Burundi ilitumbukia katika machafuko tangu mwezi Aprili mwaka jana, wakati chama tawala cha CNDD-FDD kilipomuidhinisha Rais Nkurunziza kugombea katika uchaguzi uliopita, hatua ambayo inatajwa na wapinzani kuwa ilikiuka makubaliano ya Arusha, Tanzania na katiba ya nchi hiyo.