Algeria yasisitiza kuhusu ulazima wa kuipa uzito kadhia ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i90812-algeria_yasisitiza_kuhusu_ulazima_wa_kuipa_uzito_kadhia_ya_palestina
Spika wa Bunge la Algeria amesisitiza juu ya ulazima wa kuzingatiwa na kupewa uzito suala la Palestina. Ibrahim Boughali ametoa sisitizo hilo katika kikao na ujumbe wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) kilichofanyika katika mji mkuu wa Algeria, Algiers.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 21, 2022 22:55 UTC
  • Algeria yasisitiza kuhusu ulazima wa kuipa uzito kadhia ya Palestina

Spika wa Bunge la Algeria amesisitiza juu ya ulazima wa kuzingatiwa na kupewa uzito suala la Palestina. Ibrahim Boughali ametoa sisitizo hilo katika kikao na ujumbe wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) kilichofanyika katika mji mkuu wa Algeria, Algiers.

Tangu mwanzo wa kadhia ya Palestina hadi sasa, Algeria imekuwa mtetezi wa haki za wananchi wa Palestina na imekuwa ikiunga mkono piganio la ukombozi wa Quds tukufu kwa njia mbalimbali.
Tangu yalipoanza mapigano kati ya wananchi wa Palestina na jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika mwezi wa Ramadhani mwaka huu, viongozi wa Algeria wamefuatilia matukio ya Quds kupitia mawasiliano na uratibu wa ndani ya mataifa ya Kiarabu.
Kwa mujibu wa Televisheni ya Al-Mayadeen, katika mazungumzo na ujumbe wa Hamas unaoongozwa na Zaher Jabarin, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati hiyo ya muqawama ya Palestina, Boughali amelaani sera za undumakuwili na akasisitiza kwamba suala la Palestina linapasa lishughulikiwe na kupewa umuhimu sawa na masuala mengine ya kimataifa.
Ibrahim Boughali

Katika mkutano huo, Zaher Jabarin amesisitizia shauku iliyonayo harakati ya Hamas ya kufanikiwa azimio la Algeria la maridhiano ya kitaifa lililotiwa saini na makundi ya Palestina.

Mjumbe huyo wa ofisi ya kisiasa ya Hamas pia ameiomba Algeria isaidie kulitangaza katika duru za kimataifa suala la haki za mateka Wapalestina wanaoshikiliwa katika jela za utawala ghasibu wa Kizayuni.
Kwa zaidi ya miaka 70 sasa, haki za wananchi madhulumu wa Palestina zimekuwa zikiminywa na kukandamizwa na utawala dhalimu wa Kizayuni, ambao katika kipindi chote hicho umefanya jinai za kinyama kupindukia dhidi ya wananchi hao.../