Zimbabwe kuwaadhibu wananchi wasio na 'uzalendo'
(last modified Thu, 24 Nov 2022 02:31:23 GMT )
Nov 24, 2022 02:31 UTC
  • Zimbabwe kuwaadhibu wananchi wasio na 'uzalendo'

Serikali ya Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe imeudhinisha muswada wa sheria ya kuwaadhibu wananchi wasio wazalendo, ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na vikwazo vya kiuchumi dhidi ya taifa hilo la kusini mwa Afrika.

Waziri wa Habari wa Zimbabwe, Monica Mutsvangwa aliwaambia waandishi wa habari jana Jumanne mjini Harare kuwa, Baraza la Mawaziri la nchi hiyo limepasisha muswada wa sheria hiyo inayokusudia kuwaadhibu Wazimbabwe wanaohujumu maslahi ya taifa hilo.

Sheria hiyo itakayojulikana kama "Sheria ya Uzalendo' itawaadhibu wananchi wa Zimbabwe wanaofanya lobi kwa nchi za Magharibi ili ziiwekee vikwazo nchi hiyo ya Kiafrika.

Aidha sheria hiyo inataka adhabu ya lazima kwa watu wanaopatikana na hatia katika kesi za ubakaji na mauaji, na pia imetoa tafsiri pana zaidi ya 'mihadarati hatari' mbali na kurekebisha kipengee kinachozungumzia jinai ya matumizi mabaya ya ofisi (mamlaka).   

Wazimbabwe katika maandamano ya kupinga vikwazo vya Wamagharibi

Hata hivyo vyama vya kisiasa nchini humo ukiwemo Muungano wa Wananchi wa Ajili ya Mabadiliko vimepinga sheria hiyo na kuitaja kuwa ya kifashisti na inayokanyaga katiba ya nchi.

Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) mara kwa mara imekuwa ikitoa mwito wa kuondolewa haraka na bila masharti yoyote vikwazo dhidi ya serikali ya Zimbabwe.

Vikwazo hivyo vilivyowekwa mwaka 2002 na Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya, ambavyo ni pamoja na vizuizi vya kibiashara na kifedha, vimeikwamisha Zimbabwe kuboresha uchumi wake na ustawi endelevu.