UN yaanza kufanya uchunguzi wa uvunjaji wa haki za binaadamu Burundi
Kundi moja la wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa limefanya safari nchini Burundi kwa ajili ya kufanya uchunguzi kuhusu uvunjwaji wa haki za binaadamu nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kundi hilo lilianzisha uchunguzi wake jana Jumatatu kwa lengo la kufuatilia hali ya haki za binaadamu nchini humo. Hii ni mara ya pili kwa kundi hilo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa kufanya safari nchini Burundi kwa ajili ya kazi hiyo. Hatua hiyo imekuja baada ya kuenea habari za kugunduliwa kaburi la umati, kuendelea mauaji ya kiholela kinyume cha sheria na uvunjwaji mkubwa wa haki za binaadamu, nchini Burundi. Katika duru ya kwanza ya safari yao iliyofanyika mwezi Machi mwaka huu, wataalamu hao walifanya mazungumzo na viongozi wa serikali ya Bujumbura, wajumbe wa taasisi za kiraia na viongozi wa vyama vya upinzani. Aidha safari zote za makundi hayo zinafanyika kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lililotolewa tarehe 17 Disemba mwaka jana 2015. Mbali na machafuko hayo yaliyoanza mwezi April mwaka jana kusababisha vifo vya karibu watu 500, zaidi ya watu laki mbili na elfu 50 wamekuwa wakimbizi nchini Burundi.