Kipindupindu chaua watu 51 kusini mwa Nigeria
(last modified Tue, 20 Dec 2022 07:29:42 GMT )
Dec 20, 2022 07:29 UTC
  • Kipindupindu chaua watu 51 kusini mwa Nigeria

Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na mripuko mpya wa ugonjwa wa kipindupindu kusini mwa Nigeria imeongezeka na kufikia 51.

Bernard Egbe, chifu wa jamii ya Ekureku katika eneo la Abi amesema wimbi hilo jipya la kipindupindu limeua watu 31 baina ya Jumapili na jana Jumatatu katika vijiji 10 vya jimbo la Cross River, kusini mwa nchi.

Amesema mbali na idadi ya walioga dunia kwa maradhi hayo kuongezeka kutoka 20 hadi 51, kuna watu wengine kadhaa wamelazwa hospitalini wakiwa katika hali mbaya kutokana na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Nigeria (NCDC), watu 1,569 walithibitishwa kukumbwa na ugonjwa wa kipindupindu baina mwezi Januari na Mei huko Nigeria, mbali na makumi ya wengine kuaga dunia.

Wagonjwa wa kipindupindu

Hayo yameripotiwa katika hali ambayo, katikati ya mwezi Januari mwaka huu, Wizara ya Rasilimali za Maji ya Nigeria ilisema jumla ya watu 3,598 waliaga dunia katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kutokana na ugonjwa wa kipindupindu mwaka jana wa 2021.

Janga hilo la kipindupindu limeendelea kuchukua roho za watu nchini Nigeria katika hali ambayo, ni asilimia 14 tu ya wananchi wa nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 200 ndio wenye uwezo wa kupata maji safi na salama. Hayo ni kwa mujibu wa takwimu rasmi za serikali za mwaka juzi 2020.