RSF yafanya shambulio la kwanza la droni Port Sudan
(last modified Sun, 04 May 2025 07:43:27 GMT )
May 04, 2025 07:43 UTC
  • RSF yafanya shambulio la kwanza la droni Port Sudan

Msemaji wa jeshi la Sudan ametangaza leo kuwa wanamgambo wa kikosi cha RSF wamefanya shambulio la ndege isiyo na rubani (droni) katika kambi ya jeshi la nchi hiyo na katika vituo vingine karibu na uwanja wa ndege wa Port Sudan. Hili ni shambulio la kwanza kuwahi kufanywa na wanamgambo wa RSF katika mji huo wa bandari wa mashariki.

Msemaji wa jeshi la Sudan amesema hadi sasa hakuna taarifa yoyote kuhusu watu waliouawa au kujeruhiwa katika shambulio hilo la RSF. Kwa upande wao wanamgambo wa RSF hawajatoa maelezo yoyote kuhusu kuhusika kwao katika hujuma hiyo huko Port Sudan. 

Inafaa kuashiria hapa kuwa, wanamgambo wa RFS hadi sasa wameshambulia vituo kadhaa vya kusambaza umeme katika maeneo yanayodhibitiwa na jeshi la Sudan, katikati na kaskazini mwa nchi hiyo. 

Shambulio la ndege isiyo na rubani la kikosi cha RSF huko Port Sudan linaashiria mabadiliko makubwa katika vita vya kuwania madaraka vya miaka miwili kati ya jeshi la Sudan na RSF.

Port Sudan, ambako kuna uwanja mkubwa wa ndege wa nchi hiyo ni makao makuu ya jeshi na bandari na mji huo unahesabiwa kuwa sehemu salama zaidi katika taifa hilo lililokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.