Rwanda yashambulia ndege ya kivita ya DRC kwa 'kukiuka' anga yake
(last modified Wed, 25 Jan 2023 11:52:32 GMT )
Jan 25, 2023 11:52 UTC
  • Rwanda yashambulia ndege ya kivita ya DRC kwa 'kukiuka' anga yake

Serikali ya Kigali imesema imechukua 'hatua za kujilinda' baada ya ndege ya kijeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kukiuka anga ya Rwanda.

Yolande Makolo, Msemaji wa Serikali ya Rwanda amesema katika taarifa kuwa, ndege ya kijeshi ya Sukhoi-25 ya DRC jana Jumanne adhuhuri ilikiuka anga ya Rwanda kwa mara ya tatu sasa, na kwamba Kigali imechukua hatua za kujihami kujibu uchokozi huo.

Rwanda imetoa taarifa hiyo baada ya video kusambaa katika mitandao ya kijamii, ikionyesha ndege ya kijeshi ya Sukhoi-25 ya DRC ikishambuliwa kwa kifaa kinachoonekana kama roketi au kombora, baada ya kupaa katika anga za chini juu ya Ziwa Kivu, kabla ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Goma huku ikiwa bado inateketea.

Video hiyo inaonesha wazima moto walifanikiwa kuuzima moto huo, lakini ndege hiyo imeharibiwa vibaya na moto huo. Rwanda inadai kuwa, kesi mbili za DRC kukiuka anga ya nchi hiyo zilitokea Novemba na Disemba mwaka uliomalizika.

Hii ni katika hali ambayo, Kinshasa imekanusha madai kuwa ndege ya DRC imeruka katika anga ya Rwanda, huku ikiishambulia kwa maneno makali Kigali kwa kushambulia ndege hiyo, na kusema kuwa kitendo hicho ni sawa na vita. 

Rais Paul Kagame wa Rwanda (kulia) na mwenzake wa DRC, Felix Tshisekedi

Mvutano wa kidiplomasia kati ya Rwanda na DRC unazidi kupamba moto, baada ya Kigali kuituhumu Kinshasa kwamba, inavuruga jitihada za kikanda zinazoendelea za kuleta amani mashariki mwa nchi hiyo.

Mgogoro baina ya mataifa hayo mawili jirani umeingia katika hatua mpya baada ya serikali ya Kigali kudai kwamba, Jamhuuri ya Kidemokrasia ya Kongo inajiandaa kwa vita kwa kuwaajiri mamluki wa kigeni.

Wakati Rwanda ikitoa tuhuma hizo, serikali ya Kongo DR nayo imeendelea kuinyooshea kidole cha lawama Kigali kwamba, ndio mvurugaji wa amani na usalama mashariki mwa DRC. Kongo inaituhumu jirani yake mdogo Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi la waasi wa M23, madai ambayo yamekanushwa na Rwanda, lakini yanaungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Ubelgiji na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.

Tags