Vijana: Wanasiasa ndio chanzo cha mizozo na matatizo Afrika
(last modified Fri, 17 Jun 2016 04:44:22 GMT )
Jun 17, 2016 04:44 UTC
  • Vijana: Wanasiasa ndio chanzo cha mizozo na matatizo Afrika

Idadi kubwa ya vijana barani Afrika wanahisi kuwa chimbuko la matatizo, mikwaruzano na migogoro katika nchi za bara hilo imetokana na wanasiasa wenye uchu wa madaraka na ubinafsi.

Utafiti wa maoni uliofanywa na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umeonyesha kuwa, asilimia 50 ya vijana 86,000 waliohusishwa kwenye utafiti huo wamesema uroho na uchu wa madaraka wa wanasiasa katika nchi za bara hilo ndio sababu kuu ya mizozo ya kila mara barani humo, licha ya utajiri mkubwa wa rasilimali na fursa za kuwekeza barani humo. Vijana wawili kati ya watatu waliohojiwa katika utafiti huo wa UNICEF wamesema marais wa nchi za Afrika sharti wachukue hatua za makusudi kukomesha migogoro hiyo. Ripoti ya utafiti huo ilitolewa jana Alkhamisi wakati wa maadhiisho ya Siku ya Mtoto wa Kiafrika.

Nkosazana Dlamini Zuma, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema kuhusiana na utafiti huo kuwa: "Wakati umefika kwa viongozi wa bara hili kusikiliza sauti za vijana iwapo wanataka kusimamisha sauti za risasi."

Utafiti huo ulilenga vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 30 katika nchi tofauti za bara Afrika, kuanzia Cameroon hadi Jamhuri ya Afrika ya Kati na kuanzia Mali hadi Nigeria.

Tags