Jan 30, 2023 11:46 UTC
  • Watu 15 wauawa katika shambulizi la ADF mashariki mwa DRC

Kwa akali watu 15 wameuawa katika wimbi jipya la mashambulizi yaliyofanywa na genge la wanamgambo wa ADF mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Dieudonne Malangai, afisa wa serikali katika eneo hilo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, wapiganaji wa ADF jana Jumapili walishambulia vijiji kadhaa mashariki mwa DRC na kuua watu wasiopungua 15.

Malangai amebainisha kuwa, maiti saba zimepatikana katika kijiji cha Manyala, na nane zikiwemo saba za wanawake zimepatikana katika kijiji jirani cha Ofay katika mkoa wa Ituri, karibu na mpaka wa Rwanda.

Afisa huyo wa serikali katika eneo hilo ameongeza kuwa, magaidi wa ADF wameshambulia pia kijiji cha Bandibese, lakini wamekabiliwa vikali na wanajeshi wa serikali, na hivyo hakuna maafa yaliyoripotiwa.

Haya yanajiri wiki moja baada ya shambulio jingine la silaha lililofanywa na kundi hilo la kigaidi kuua watu 24, aghalabu yao wakiwa askari huko mashariki mwa Kongo DR.

Magaidi wa ADF wenye asili ya Uganda

ADF iliundwa miaka ya 1990 kama kundi la waasi nchini Uganda. Kundi hilo la kigaidi linaendesha harakati zake katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pia. Vijiji vya Kongo huvamiwa na kuporwa mara kwa mara na kundi hilo la waasi wa Uganda wa ADF.

Kundi hilo linashutumiwa kwa kuua maelfu ya watu katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri nchini Kongo na kuhusika na mashambulizi ya mabomu nchini Uganda mwaka 2021.

Tags