Jun 17, 2016 08:23 UTC
  • Waasi wa Uganda waendelea kufanya uhalifu CAR

Mkuu wa mkoa wa mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati ametangaza kuwa waasi wa kundi la Lord's Resistance Army (LRA) kutoka Uganda wameteka nyara watu 17 na kuwapeleka kusikojulikana.

Ghislain Kolengo ambaye ni mkuu wa mkoa wa Haut-Mbomou amesema kuwa waasi wa LRA wamevamia kijiji cha Kadjema na kuteka nyara raia 17 wa kijiji hicho.

Ripoti zinasema kuwa waasi wa kundi la Lord's Resistance Army kutoka Uganda wamezidisha uhalifu na kutenda jinai katika Jamhuri ya Afrika ya Kati hususan baada ya jeshi la Uganda kutangaza kuwa, litawarejesha nyumbani askari wake waliokuwa wakiongoza mapambano dhidi ya kundi hilo.

Mwaka jana pekee kundi hilo linalopigana na serikali ya Rais Yoweri Museveni kwa shabaha eti ya kuanzisha utawala kwa mujibu wa amri kumi za Biblia, liliteka nyara watu wasiopungua 350 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wakiwemo watoto na wanawake wanaolazimishwa kuhudumia wapiganaji wa kundi hilo kama watumwa wa ngono.

Tags