Mar 17, 2023 07:02 UTC
  • Ugonjwa usiojulikana wazua wasiwasi mkoani Kagera, Tanzania, waua watu watano

Serikali ya Tanzania imetoa tahadhari juu ya uwepo wa ugonjwa ambao bado haujajulikana Mkoani Kagera katika Wilaya ya Bukoba Vijijini ambapo watu 7 wanasadikika walipata dalili za homa, kutapika, kutokwa damu maeneo mbalimbali ya mwili na figo kushindwa kufanya kazi.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya ya Tanzania imesema watu watano kati ya saba waliopatwa na ugonjwa huo usiojulikana wamefariki dunia, na wengine wawili wako hospitali wanakoendelea kupata matibabu.

Mganga Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Prof. Tumaini Nagu ametoa taarifa hiyo katika Ofisi za Wizara Jijini Dodoma. Amesema Wizara ya Afya imepokea taarifa za uwepo wa ugonjwa ambao bado haujajulikana huko Kagera, Bukoba Vijijini, Kata ya Maruku na Kanyangereko, Vijiji vya Bulinda na Butayaibega. Amesema mwenendo wa ugonjwa huo unaashiria uwezekano kuwa ni ugonjwa wa kuambukiza, hivyo Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu na kuchukua hatua za kuudhibiti ili usisambae.

Prof. Nagu amewataka wananchi kuwahi kwenye vituo vya huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu endapo wataona dalili kama kupatwa na homa, kutapika, kuharisha, kutoka damu na mwili kuishiwa nguvu.

Mwezi Julai mwaka jana pia Waziri wa Afya wa Tanzania Ummy Mwalimu alitangaza kuwa: “Kuna mlipuko wa ugonjwa usiojulikana Kusini mwa Tanzania (Lindi) na kwamba sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa wagonjwa zimeonyesha kuwa siyo ugonjwa wa Ebola, Maburg wala Uviko19. Ugonjwa huo ulisababisha vifo vya watu watatu.

Ummy Mwalimu

Baadaye Wizara ya Afya ya Tanzania ilitangaza kuwa vipimo vimethibitisha kuwa mlipuko huu ni wa ugonjwa wa Leptospirosis, Field Fever unaojulikana kwa lugha ya Kiswahili kama Homa ya Mgunda.

Tags