Matokeo ya mashambulizi dhidi ya wafuasi wa Sheikh Zakzaky nchini Nigeria
Mashinikizo dhidi ya Waislamu wa Nigeria na wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky bado yanaendelea. Kuhusiana na hilo, vikosi vya usalama katika jimbo la Kaduna vimewaua watu wasiopungua 6 katika shambulio dhidi ya wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
Mauaji hayo yametokea baada ya wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria kufanya maandamano ya amani wakiiomba serikali imrudishie Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe pasipoti zao ili waweze kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupokea matibabu ya dharura.
Sheikh Ebrahim al-Zakzaky na mkewe ambao walikamatwa tarehe 13 Disemba 2015 katika shambulio la jeshi la Nigeria dhidi ya kituo chao cha mafunzo ya kidini au kwa jina jingine Husseiniyah katika mji wa Zaria, waliachiliwa huru baada ya kustahimili kifungo cha miaka mingi jela. Hata hivyo kutokana na mashinikizo ya mazingira ya jela na kutozingatiwa taratibu za matibabu sehemu hiyo, hali yao ya kiafya imezorota kwa kadiri kwamba Sheikh Zakzaky ameendelea kudhoofika hivyo anatakiwa kuhamishiwa nje ya Nigeria kwa ajili ya kupata matibabu zaidi.
Kuhusiana na hilo, waandamanaji wa Nigeria wameiomba serikali imrudishie hati yake ya kusafiria ili aweze kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu na kudhaminiwa dawa. Wataalamu wa tiba wanasisitiza kuwa matibabu maalumu anayohitajia Sheikh Zakzaky yanapatikana tu nje ya Nigeria.
Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya Abuja imezidisha mashinikizo dhidi ya Waislamu kadiri kwamba imepiga marufuku shughuli zao za kidini kama vile Tasua na Ashura za kukumbuka mauaji ya Imam Hussein (as), ambaye ni mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw) na vilevile kuzuia sherehe zao za furaha zinazojumuisha mikusanyiko mikubwa. Kwa hakika, katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya Nigeria imejaribu kupunguza au kuondoa kabisa uwepo wa Waislamu katika nyanja mbalimbali za kijamii na kisiasa nchini humo lakini bila mafanikio makubwa hadi sasa.
Chimbuko la kushadidi siasa za serikali ya Nigeria dhidi ya Waislamu linaweza kuonekana wazi katika mabadiliko ya ndani ya kisiasa, uga wa kimataifa, uingiliaji kati wa kigeni, maliasili na nafasi ya nchi hiyo katika eneo la magharibi mwa Afrika. Kwa hakika, serikali ya katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ikikabiliana na Waislamu kwa mtazamo wa tishio la kiusalama. Ushawishi na mashinikizo ya utawala haramu wa Israel na washirika wake kwa serikali ya Nigeria yamewapelekea Waislamu kukabiliwa na mashinikizo makali kutoka kwa serikali kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Kwa mtazamo wa utawala huo ghasibu na washirika wake, uwepo wa Waislamu wenye nguvu nchini Nigeria ni kikwazo kikubwa cha kuendelezwa uhusiano na kufikiwa malengo yake ya kimaslahi, ikiwa ni pamoja na uporaji wa maliasili muhimu na utajiri wa mafuta ya nchi hiyo ya Kiafrika.
Akiashiria kwamba mauaji ya Zaria yalitekelezwa kwa amri ya Washington na washirika wake, Sheikh Zakzaky amesema: "Harakati hii itafuatilia kesi iliyowasilishwa na Jumuiya ya Haki za Waislamu ya London katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC."
Licha ya mashinikizo hayo, Waislamu wa Nigeria wamekuwa wakifanya maandamano katika miji tofauti ya nchi hiyo, wakimuunga mkono Sheikh Zakzaky, na kuitaka serikali isaidie kutibu na kumruhusu asafiri nje ya nchi kwa ajili ya kupatiwa matibabu yanayofaa.
At-Tasafi, mjumbe wa timu ya madaktari wa Sheikh Zakzaky anasema kuhusiana na hilo: Serikali ya Nigeria haimuruhusu Sheikh atibiwe nje ya nchi kwa hofu kuwa huenda akaibua mapinduzi mengine ya Kiislamu baada ya kurejea nchini.
Licha ya mabadiliko ya kisiasa nchini Nigeria, lakini bado viongozi wa nchi hiyo hawana mtazamo mzuri kuhusu Waislamu. Hasa ikitiliwa maanani kuwa baadhi ya viongozi wa majimbo ndio wanaotoa maamuzi ya mwisho kuhusu masuala muhimu yanayohusu majimbo yao. Kwa mfano siku chache zilizopita Gavana wa Jimbo la Kaduna “Nasiro el-Rufai”, aliahidi kwamba iwapo mgombea wake atafanikiwa kushinda uchaguzi wa ugavana, atamaliza kazi ambayo haijakamilika ya kuondoa na kuwafuta kabisa wanachama wa Kishia wa Harakati ya Kiislamu katika jimbo hilo. Inaonekana wazi kuwa wameazimia kikamilifu kuendeleza hatua za kuwakandamiza Waislamu wa Nigeria.