AU yazitolea wito pande hasimu Burundi kufanya mazungumzo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9565-au_yazitolea_wito_pande_hasimu_burundi_kufanya_mazungumzo
Wawakilishi wa Umoja wa Afrika (AU) katika mgogoro wa kisiasa wa Burundi wamezitolea wito pande zinazozozana katika mgogoro wa nchi hiyo kutatua hitilafu zao kwa njia ya mazungumzo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 19, 2016 22:50 UTC
  • AU yazitolea wito pande hasimu Burundi kufanya mazungumzo

Wawakilishi wa Umoja wa Afrika (AU) katika mgogoro wa kisiasa wa Burundi wamezitolea wito pande zinazozozana katika mgogoro wa nchi hiyo kutatua hitilafu zao kwa njia ya mazungumzo.

Ripoti kutoka Kampala mji mkuu wa Uganda zinasema kuwa Rais Yoweri Museveni wa nchi hiyo na Benjamin Mkapa Rais Mstaafu wa Tanzania ambao wanafanya juhudi kama wasuluhishi katika mgogoro wa Burundi, jana walikutana na kufanya mazungumzo katika ikulu ya Rais wa Uganda.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wawili ambao ni wasuluhishi wa Umoja wa Afrika katika mgogoro wa Burundi wametoa taarifa na kuvitaka vyama na makundi hasimu ya Burundi kuheshimu vipengee vya makubaliano ya Arusha ambayo yalihitimisha vita vya ndani vya nchi hiyo kuanzia mwaka 1993 hadi 2005. Benjamin Mkapa na Yoweri Museveni wamezitaka pande zinazozozana Burundi kujongea kwenye meza ya mazungumzo na kutatua hitilafu zao kwa njia ya amani. Mazungumzo ya kusaka amani Burundi ambayo yalipangwa kufanyika mwezi Januari uliopita mjini Arusha Tanzania, hayakufanyika kufuatia serikali ya Burundi kupinga suala hilo.