Al-Azhar yawataka Waislamu kuulinda Msikiti wa Al-Aqsa
Taasisi ya Al-Azhar ya Misri imetoa wito kwa Waislamu wote kuulinda na kuutetea Msikiti wa Al-Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Msikiti wa Al-Aqsa, ukiwa ni nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu-Kipalestina wa mji wa Quds, daima umekuwa mlengwa wa vitendo vya uharibifu vya utawala haramu wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu.
Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar cha Misri kimetoa wito kwa Waislamu wote duniani kuulinda Msikiti wa Al-Aqsa, kusimama kidete kwenye safu moja kwa ajili ya kutetea eneo hilo takatifu na kuzuia hujuma za wale wanaofanya njama dhidi ya Msikiti wa Aqsa na viwanja vyake.
Katika siku za hivi karibuni, jeshi la utawala wa Kizayuni limeongeza hujuma na mashambulizi dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa na waumini wa Kipalestina na kuwatia mbaroni karibu watu 400.

Siku ya Jumatano iliyopita, vikosi vya utawala haramu wa Israel vilivamia eneo hilo takatifu kwa mara ya pili mfululizo wakafanya uharibifu na jitihada za kuwafukuza waumini wa Kipalestina katika Msikiti wa Al Aqsa kwa kurusha maguruneti na kuwamiminia risasi za plastiki.
Nchi za Kiislamu zimelaani vikali uchokozi huo wa Wazayuni na kutoa wito kwa taasisi za kimataifa kusitisha jinai za Israel na kulinda jengo la Msikiti wa al-Aqsa.