Apr 16, 2023 10:26 UTC
  • Mapigano ya kuwania madaraka baina ya majenerali yaingia siku ya pili nchini Sudan

Mapigano kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Radiamali ya Haraka yameingia siku ya pili, huku milipuko ikisikika tangu alfajiri ya leo, Jumapili, karibu na Mji wa Michezo, kusini mwa mji mkuu, Khartoum.

Hali ya sintofahamu inaendelea kutanda kuhusu yanayojiri katika medani ya vita kutokana na taarifa zinazokinzana zinazotolewa na pande hasimu. Hadi sasa watu zaidi ya 56 wameripotiwa kuuawa na wengine zaidi ya 600 kujeruhiwa katika mapigano hayo ya ndani.

Kufuatia hali ya utulivu iliyotanda mji mkuu wa Sudan nyakati za siku wa kuamkia leo Jumapili, ripoti zinasema kuwa milipuko imesikika tangu mapema alfajiri mjini Khartoum, huku moshi mkubwa ukitanda anga ya mji huo.  

Habari za kugongana zinahusiana zaidi na Kamandi Kuu ya jeshi la Sudan ambapo mshauri wa kisiasa wa Vikosi vya Radiamali ya Haraka ameiambia televisheni ya Al-Jazeera ya Qatar kwamba: Mapigano makali yanaendelea ndani ya makao Makuu ya Kamandi ya Jeshi, na kwamba maafisa wengi wamejiunga na kikosi hicho. Hata hivyo, msemaji wa Jeshi la Sudan amekanusha kile alichokiita madai ya waasi ya kuzingirwa kwa Kamandi Kuu mjini Khartoum.

Mapigano hayo yalizuka baada ya mvutano kuhusu pendekezo la kuanzishwa utawala wa kiraia na kuunganishwa vikosi vyote ndani ya jeshi moja la taifa.

Jeshi la Sudan na wapinzani wake, Rapid Support Forces (RSF), wanadai kudhibiti uwanja wa ndege na maeneo mengine muhimu mjini Khartoum na miji ingine ya nchi hiyo, ambako mapigano yameendelea usiku kucha.

Kamati ya madaktari ya Sudan ilisema mapema leo kuwa, raia wasiopungua 56 wameuawa katika miji na mikoa mbalimbali ya nchi hiyo, na kwamba makumi ya wanajeshi pia wameuawa. 

Wafanyakazi 3 wa Shirika la Chakula Duniani (WFP), waliuawa baada ya RSF na wanajeshi kufyatuliana risasi katika kambi ya kijeshi huko Kabkabiya, magharibi mwa Sudan.

Mapigano ya sasa nchini Sudan ni kati ya vitengo vya jeshi vinavyomtii kiongozi mkuu, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na vikikosi vya RSF, vinavyoongozwa na naibu kiongozi wa kijeshi wa Sudan, Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana pia kama Hemedti.

Mohamed Hamdan Dagalo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amezungumza na Jenerali Burhan na Jenerali Dagalo, akiwataka kukomesha ghasia.

Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lilitarajiwa kufanya mkutano leo kujadili hali ya mambo nchini Sudan.

Tags