Sheikh Zakzaky alishukuru taifa la Iran kwa kuwasaidia wanaodhulumiwa
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria anayeshikiliwa na jeshi la nchi hiyo amewashukuru wananchi wa Iran kwa kuwafikishia walimwengu ujumbe wa kudhulumiwa na kukandamizwa wa harakati hiyo.
Katika ujumbe wake uliosomwa na baadhi ya jamaa zake waliokwenda kumtembelea jela, Sheikh Ibrahim Zakzaky ameshukuru juhudi zinazofanywa na watu katika nchi mbalimbali hususan taifa la Iran na wanaharakati wa Kiislamu wanaoiunga mkono Harakati ya Kiislamu.
Watu waliokutana na Sheikh Ibrahim Zakzaky wanasema jicho lake la kushoto limepofuka na kwamba juhudi za kutibu jicho lake la kulia zimekuwa na mafanikio ya kiwango fulani. Kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria aliteswa na kupigwa risasi kadhaa Disemba mwaka uliopita baada ya jeshi la Nigeria kushambulia nyumba yake katika mji wa Zaria katika jimbo la Kaduna. Mamia ya Waislamu wasio na hatia pia waliuawa katika mashambulizi hayo.