Polisi Burundi yawakamata wafanya magendo ya binadamu
Polisi ya Burundi imewatia nguvuni watu kadhaa kwa tuhuma za kushiriki katika magendo ya binadamu.
Msemaji wa polisi ya Burundi, Pierre Nkurikiye amesema kuwa watu 7 wakiwemo raia watatu wa Burundi na 4 wa Kenya wametiwa nguvuni tangu mwezi Aprili hadi sasa nchini humo kwa tuhuma za kushiriki katika magendo ya wanawake. Nkurikiye ameongeza kuwa, watu hao saba ni wanachama wa mtandao wa magendo ya binadamu na wanayafanyia kazi mashirika 4 ya Saudi Arabia, mashirika mengine 2 ya Oman, makampuni mawili ya Burundi na shirika moja la Kenya.
Msemaji wa polisi ya Burundi amesema kuwa, hadi sasa wanawake na wasichana 267 wametoroshwa nchini Burundi na kupelekwa katika nchi za Saudi Arabia, Oman na Lebanon.
Kwa sasa polisi ya Burundi inamsaka mkurugenzi wa kampuni moja ya binafsi ambaye ametoroka baada ya polisi kuanza uchunguzi unaohusiana na kadhia hiyo.