May 19, 2023 10:31 UTC
  • UN yalaani ukiukwaji wa makubaliano ya kusitisha vita Sudan, mapigano makali yaripotiwa Khartoum

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu, Martin Griffiths, amelaani kile alichokitaja kuwa ukiukwaji wa mara kwa mara na mkubwa wa makubaliano yaliyofikiwa wiki moja baina ya pande zihasimu katika mzozo wa Sudan ya kulinda maisha ya raia, harakati za misaada ya kibinadamu na miundombinu.

Martin Griffiths amesema hayo huku Shirika la Mpango wa Chakula Duniani likitatizika katika shughuli zake za kufikisha misaada ya kibinadamu katika angalau majimbo 6 ya Sudan . 

Mashahidi wanasema kumeshuhudiwa mashambulizi ya anga ya Jeshi la Taifa dhidi ya wapiganaji wa kikosi cha RSF katika vitongoji kadhaa vya makazi ya raia Kusini mwa Khartoum, huku kikosi cha akiba cha polisi kikipigana na RSF ardhini.

Jeshi la Taifa la Sudan linategemea zaidi nguvu za kikosi cha anga na silaha nzito katika jaribio la kuwatimua wapiganaji wa RSF ambao wameingia katika maeneo ya Khartoum na Omdurman, miiji miwili inayotenganishwa na Mto Nile.

Kwa mujibu wa mashahidi, mapigano hayo yamepanuka zaidi hadi umbali wa kilomita 1,000 Magharibi mwa Khartoum huko Nyala, moja ya miji mikubwa ya Sudan na mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini.

Ripoti zinasema kuwa sauti ya milio ya risasi, ikiwa ni pamoja na vifaru, zimesikika kwa mara ya kwanza tangu kutangazwa kwa mapatano ya kusitisha mapigano hususan kwenye maeneo ya raia.

Mapigano makali katika mji mkuu, Khartoum, na viunga vyake pia yamezidisha mateso ya wagonjwa na familia zao kutokana na uhaba wa dawa, kwani makampuni husika yameacha kusambaza bidhaa hizo, viwanda vya ndani vya dawa vimeharibiwa, na maduka mengi ya dawa yamefungwa huku mengine yakiporwa.

Duka la dawa, Khartoum

Takwimu zinasema Wasudan karibu elfu moja wameuawa hadi sasa katika mapigano yanayoendelea baina ya Jeshi la Taifa linaloongozwa na mkuu wa Baraza la Utawala wa Mpito, Abdel Fattah Al-Burhan na Vikosi vya Msaada wa Haraka, chini ya uongozi wa naibu wake za wamani, Muhammad Hamdan Dagalo. Wasudani wengine wasiopungua 3500 wamejeruhiwa. 

Zaidi ya Wasudan milioni moja pia wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi. 

Tags